Mabomu yaendelea kuripuka Nigeria | Matukio ya Afrika | DW | 15.07.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mabomu yaendelea kuripuka Nigeria

Siku moja baada ya Kansela Angela Merkel kumaliza ziara yake nchini Nigeria, polisi wanane wamejeruhiwa hii leo (15 Julai 2011) mjini Maiduguri kufuatia mripuko wa bomu unaohusishwa na watu wanaofuata itikadi kali.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na mwenyeji wake Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na mwenyeji wake Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria

Msemaji wa kikosi kinachosimamia operesheni katika mji huo ulioko kakskazini mashariki mwa Nigeria, Kanali Victor Ebhaleme, amesema kuwa ishara zinaonesha bomu hilo lilitegwa na wanamgambo wa kundi la Boko Haram, ambalo limekuwa likihusika na mashambulizi na namna hiyo.

Mji wa Maiduguri umekuwa ukikumbwa na matukio ya miripuko ya mabomu pamoja na mashambulio ya risasi, karibu kila siku mnamo wiki za hivi karibuni, ambapo kundi la Boko Haram linashutumiwa kufanya mashambulio hayo. Boko Haram lilianzisha uasi mwaka 2009.

WHO yaonya kipindupindu Ethiopia

Mama akimbeba mtoto wake mwenye dalili za kipindupindu

Mama akimbeba mtoto wake mwenye dalili za kipindupindu

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kwamba kiasi ya watu milioni 5 wako katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya kipindupindu nchini Ethiopia, kutokana na ukame mbaya kuikumba nchi hiyo. Kutokana na uhaba wa maji, ugonjwa wa kuhara umeripuka katika maeneo ya watu wengi.

Akizungumza mjini Geneva, msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic, amesema kwa ujumla kiasi ya watu milioni 8.8 nchini Ethiopia wanakabiliwa na tishio la ugonjwa wa malaria, ambapo milioni 5 miongoni mwao wanakabiliwa pia na tishio la kipindupindu.

Shirika hilo limesema ukame mbaya kabisa umelikumba eneo la pembe ya Afrika, ambapo hivi sasa zaidi ya watu milioni 11 wa nchi za Ethiopia, Kenya, Djibout na Somalia, wanakabiliwa na kitisho cha maradhi ya kuambukiza kama vile kipindupindu, surua na ugonjwa wa kupooza.

Mbali ya kukimbia mapigano katika nchi yao, wakimbizi kutoka Somalia wamekuwa wakimiminika katika kambi ya Dadaab nchini Kenya kutokana hali mbaya ya ukame nchi mwao.

Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, jana alitangaza kufunguliwa kwa kambi nyingine huko Dadaab kukabiliana na wimbi hilo.

Kamishna wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Antonio Guterres, amempongeza Odinga kwa hatua hiyo.

Maandamano makubwa yaendelea Misri

Mwandamanaji akichoma picha ya kiongozi wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak

Mwandamanaji akichoma picha ya kiongozi wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak

Maelfu ya waandamanaji leo wamekusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo katika kuendeleza mbinyo wao dhidi ya Baraza Kuu la Kijeshi la Misri, kulitaka kuharakisha mageuzi na pia kumfikisha mahakamani rais wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.

Hata hivyo, kundi maarufu la upinzani nchini Misri la Ikhwanul-Muslimin (Udugu wa Kiislamu), limesema halishiriki katika mbinyo huo na kusisitiza kuwa utawala huo wa kijeshi unahitaji muda ili kwanza utekeleze matakwa ya mwanzo.

Waandamanaji pia wamekusanyika katika maeneo mengine ya Alexandria na Suez. Wandamanaji hao pia wanataka askari polisi wote wanaotuhumiwa kuhusika na utesaji na mauaji dhidi ya waandamanaji, ama kabla au wakati wa vuguvugu la umma la Januari 25 wafikishwe mbele ya sheria.

Waziri Mkuu wa Misri, Essam Sharaf, alikwishatoa amri ya kutimuliwa kwa maafisa wa juu wa jeshi la polisi wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo tokea wiki moja iliyopita, ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani, Mansur Essawy, ametangaza kuundwa upya kwa idara zilizo chini ya wizara yake.

NATO yakutana na Kundi la Mashauriano na Libya wakutana

Viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wakikutana na Kundi la Mashauriano la Libya, Istanbul

Viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wakikutana na Kundi la Mashauriano la Libya, Istanbul

Kiasi ya mawaziri na wanadiplomasia wa juu 15 leo wanakutaka mjini Istanbul, Uturuki, kujadiliana jinsi ya kupatikana kwa suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Libya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, William Hague wa Uingereza, pamoja na mawaziri wengine wa nje wa Ufaransa, Alain Juppe, na Franco Frattini wa Italia wanashiriki katika mkutano huo.

Mpango wa kumtaka kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, aondoke madarakani kwa amani, unatarajiwa kuwa miongoni mwa ajenda kuu za kikao hicho.

Mapema wiki hii, Ufaransa ilisema kuwa suluhisho la kisiasa za mzozo huo wa Libya uliodumu kwa muda wa miezi minne sasa huenda likawa njiani kufikiwa.

Mzozo wa Libya ulioanza kama uasi dhidi ya utawala wa miongo minne wa kiongozi wa nchi hiyo, hivi sasa umegeuka na vita vya umwagaji mkubwa wa damu.

Vita hivi vimeyaweka mataifa ya Magharibi katika hatua ngumu kuliko yalivyotarajia kuwa yangeliweza kumuondoa kwa urahisi madarakani Kanali Gaddafi.

Kenya yaridhia bilioni 9 kupambana na janga la njaa

Ukame na njaa vyawakimbiza watu Somalia kuingia Kenya

Ukame na njaa vyawakimbiza watu Somalia kuingia Kenya

Baraza la Mawaziri la Kenya limesema limeidhinisha matumizi ya dharura ya shilingi bilioni 9 sawa na dola milioni 100, kununua chakula kwa wahanga wa ukame nchini humo.

Janga kubwa kabisa la chakula duniani linaziandama nchi za eneo la pembe ya Afrika zikiwemo Kenya, Ethiopia na Somalia, ambapo inakadiriwa zaidi ya watu milioni 10 wanaweza kukumbwa na njaa.

Marekani yapongeza makubaliano ya Darfur

Mkutano wa kutafuta suluhu ya Darfur nchini Qatar

Mkutano wa kutafuta suluhu ya Darfur nchini Qatar

Marekani imepongeza kufikiwa kwa mkataba wa amani kati ya serikali ya Sudan na kundi la waasi wa Darfur, na kutoa wito kwa makundi mengine kuingia majadiliano ya amani.

Marekani imeishukuru Qatar iliyosimamia kutiwa saini kwa mkataba huo kati ya Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan na kundi la Liberation and Justice Movement.

Katika taarifa yake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Mark Toner, amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua moja mbele katika kuelekea kwenye suluhisho la kudumu la mzozo wa Darfur.

Hali ya magereza nchini Uganda inatisha

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda

Ripoti ya Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu Human Rights Watch inasema magereza nchini Uganda yanawatumikisha wafungwa kazi ngumu zinazofanana na utumwa.

Ripoti hiyo imesema wafungwa huandamwa na vitendo vya kubughudhiwa na unyonyaji, vinavyofanywa na maafisa wa magereza.

Kwa mujibu wa Shirika hilo, wafungwa huchapwa viboko au kuchomwa moto wanapojaribu kuepuka kufanya kazi ngumu.

Mtafiti wa Human Rights Watch, Katherine Todrys, amesema wafungwa nchini Uganda, ambao wengi hawajahukumiwa kwa uhalifu wowote, hupigwa vibaya.

Kiasi ya wafungwa 17,000, ambao ni zaidi ya nusu ya wafungwa wote nchini humo, bado hawajahukumiwa, wakati wafungwa kwa jumla wakilazimishwa kulala kwa zamu, kwa sababu ya kujaa kwa magereza. Hali zao ni mbaya na hakuna matibabu wala chakula bora.

Todrys amesema ni wafungwa chache tu wanaougua Ukimwi na kifua kikuu ambao hupewa huduma ya kutosha.

Mambo si shwari kwenye serikali ya pamoja ya Zimbabwe

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, na Waziri Mkuu wake, Morgan Tsavingarai

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, na Waziri Mkuu wake, Morgan Tsavingarai

Chama cha Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, (MDC), kimeyapuuza madai ya chama cha Rais Robert Mugabe ZANU-PF kutaka uchaguzi mkuu ufanyike mwaka huu, licha ya Mugabe kukubali hapo awali ratiba ya mwaka 2012.

Msemaji wa MDC, Douglas Mwozorta, amepuuza wito huo na kuongeza kuwa kwanza chama cha ZANU PF ni lazima kikamalishe mageuzi ya demokrasaia waliyokubaliana.

Mwonzora ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani (DPA), kwamba uchaguzi utafanyika tu chini ya katiba mpya.

Wiki iliyopita wawakilishji kutoka MDC na ZANU-PF walikubaliana ratiba ya kufanyika uchaguzi mwaka 2012 na kurefusha muda wa serikali yao ya muungano hadi mwaka ujao.

Kwa mujibu wa makubaliano ya kugawana madaraka kati ya Mugabe na Tsvangirai ya mwaka 2008, Zimbabwe inapaswa kuwa na katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu utakaomaliza kuwepo kwa serikali ya muungano. Kura ya maoni kuhusu katiba mpya sasa imepangwa kufanyika Septemba mwaka huu, badala ya mpango wa awali wa kutaka kuitisha kura hiyo Novemba mwaka jana.

Mwandishi: Aboubakar Liongo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman