1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya mawaziri nchini Uganda yazusha mjadala mseto

Lubega Emmanuel DW Kampala.16 Desemba 2019

Mageuzi aliyofanya rais Museveni wa Uganda kwenye baraza la mawaziri mwishoni mwa juma yameibua maoni mseto miongoni mwa wanasiasa na wananchi.

https://p.dw.com/p/3UuO6
Yoweri Museveni
Picha: picture-alliance/dpa/A. Novoderezhkin

Mageuzi aliyofanya rais Museveni wa Uganda kwenye baraza la mawaziri mwishoni mwa juma yameibua maoni mseto miongoni mwa wanasiasa na wananchi. Huku wakijadili vigezo alivyotumiwa kuwatimua mawaziri saba, wengi wanashangaa kuhusu uteuzi wa wanasiasa wa upinzani kuwa miongoni mwa baraza lake la mawaziri.

Mageuzi kwenye baraza la mawaziri la Uganda ndiyo yametawala gumzo za kisiasa hata kwenye majukwaa ya kijamii nchini Uganda. Hii ni kufuatia hatua ya rais Museveni kuwatupa nje mawaziri kadhaa na pia kuwahamisha baadhi hadi kwenye wizara ambazo kwa wengi hawastahiki. Kuna maoni kwamba baada ya kuongoza maandamano ya kupambana na ufisadi, Museveni ameamua kuwaondoa mawaziri wake ambao inadaiwa wamehusika pakubwa katika maovu hayo.

Mkewe Rais Museveni bi Janet Museveni ni miongoni mwa wale ambao walibaki katika nyadhifa zao za uwaziri.
Mkewe Rais Museveni bi Janet Museveni ni miongoni mwa wale ambao walibaki katika nyadhifa zao za uwaziri.Picha: Getty Images/AFP/J. Watson

Lakini pia kuna mtazamo wa wengine juu ya vigezo vya uteuzi na pia sababu za kuwatupa nje mawaziri kadhaa. Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa hii ni mojawapo ya mikakati ya Rais Museveni akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Uteuzi wa mbunge Raphael Magyezi kuwa waziri wa serikali za mitaa kama waziri wa mitaa nao umeibua mjadala wa kipekee. Yeye ndiye aliyewasilisha muswaada wa kuondoa ukomo wa umri wa mgombea urais na hivyo kumwezesha rais wa sasa kuwa na fursa nyingine ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao. Uteuzi wake umetafsiriwa kuwa zawadi na pengine ahadi ambayo imetimizwa licha ya muda mrefu. Wanasiasa wa upinzani wanashangaa kwa nini watu kama yeye wasio na ujuzi muafaka wapewe nyadhifa za uwaziri.

Kuna dhana kwamba baadhi ya mawziri waliopinga hatua ya kuondoa ukomo wa umri na kuonekana wakishirikiana na upinzani wamelengwa katika mageuzi hayo.Mageuzi hayo kwenye baraza la mawaziri yamebiriwa na wanasiasa waliotarajia angalau safari hii rais Museveni angewapa nafasi kutokana na utendaji kazi wao.