Maandamano Nairobi kupinga mradi wa mkaa wa mawe Lamu | Matukio ya Afrika | DW | 12.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Maandamano Nairobi kupinga mradi wa mkaa wa mawe Lamu

Mamia ya waandamanaji wamejitokeza katika barabara za Nairobi kupaza sauti zao kwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, wakipinga mradi wa mkaa wa mawe katika kaunti ya Lamu.

Waandamanaji hao waliotokea kaunti za Lamu na Kitui walishirikiana na asasi ya Greenpeace Africa kupinga mradi wa mkaa wa mawe ambao utahitaji uwekezaji wa dola bilioni mbili na kuzalisha umeme wa megawati 1050. Maandamano yao yalianzia katika bustani ya Uhuru hadi kwenye wizara ya kawi na baadaye wakakamilishia katika ubalozi wa China.

Wanasema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya China, ni hatari kwa mazingira na pia gharama yake ni ya juu sana. Mohammed Mbwana ambaye ni mkazi wa Lamu, amesema, "kitu cha kwanza tunapinga ni uchafuzi wa mazingira, maanake matokeo yake hayatakuwa mazuri, jambo la pili, wakazi kwenye mradi huu, hawakuhusishwa hii ina maanisha kuwa wanatunyanyasa, ndio maana tunapinga leo kwa kufanya maandamano.”

Mbwana amesema kuwa hawatakubali mradi huo uendelee kwa kuwa katiba inamlinda mwananchi. "Tunaomba dunia iungane na sisi, mataifa mengi yanaancha kutumia mkaa wa mawe, kwanini nasi tunarudi nyuma walikotoka?”

Ameongeza kusema kuwa baadhi ya watu kwenye mradi huu wanatumia mbinu chafu kutimiza maslahi yao bila kujali maslahi ya wananchi wengi. "Serikali ilipaswa kushirikisha wananchi kwenye mradi huu.”

Yamkini thuluthi mbili ya wananchi wa Kenya hutumia umeme ambao unatokana na nishati mbadala. Rais Uhuru Kenyatta amewahi kunukuliwa akisema kuwa atahakikisha kuwa taifa linatumia nishati mbadala kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2020. Huku haya yakifanyika wizara ya Fedha imejumuisha kwenye bajeti yake mradi huu kuendelea.

Wakaazi wa Lamu wanaandamana pia kwa sababu hawakuhusishwa kwenye suala la mradi huo

Wakaazi wa Lamu wanaandamana pia kwa sababu hawakuhusishwa kwenye suala la mradi huo

Iwapo mradi huu utaendelea kama ilivyopangwa, huenda vivutio vya utalii hasa katika Pwani ya Kenya vikaathiriwa. Samia Omar mwenye umri wa miaka 45 ambaye ni miongoni mwa waandamanaji amesema:

"Kwa hivyo tunaiambia serikali ya Kenya, iheshimu raslimali za utalii maana hizo ndizo huvutia watalii kuja Kenya. Tunajua kwamba mradi wa mkaa wa mawe umekataliwa ulimwenguni mzima, lakini kwa sababu ya maslahi ya watu wachache, wanataka kuangamiza kizazi kijacho. Hiyo hatutakubali.”

Omar amemaliza kwa kusema, "mradi huu umeleta maafa. Marekani, China, Ujerumani na Japani zimekataa mradi huu kwa sababu ya athari yake kwa tabia nchi."

Wataalamu wameonya kuwa iwapo serikali itaendelea kutekeleza mradi huo huenda ukawa na matokeo hasi kama ule wa reli ya kisasa ambapo mlipa kodi atalazimishwa kulipia deni la dola bilioni nane.

Wataalamu wameonya kuwa iwapo serikali itaendelea kutekeleza mradi huo huenda ukawa na matokeo hasi

Wataalamu wameonya kuwa iwapo serikali itaendelea kutekeleza mradi huo huenda ukawa na matokeo hasi

Mwaka 2017, kampuni ya China Power Global ilisaini mkataba wa dola bilioni mbili ambazo ni sawa na shilingi bilioni 200 za Kenya na kampuni ya Amu Power kwa ujenzi wa mradi huo, huku benki ya China ikikubali kufadhili dola bilioni 1.2 ikiwa ni sawa na shilingi bilioni120 za Kenya kwenye mradi huo.

Waandamanaji wanahofu kuwa taifa linakiuka malengo yake ya kupigia debe nishati mbadala na badala yake kushabikia nishati yenye kuchafua mazingira kwa asilimia 700.

Kichekesho ni kuwa China imejitolea kupunguza matumizi ya nishati ya mkaa wa mawe kwa robo moja lakini inatumia mataifa mengine kufikia malengo yake.

Lamu ni mji wenye historia ya zaidi ya miaka 700 ambao ulitambuliwa na Umoja wa Mataifa UNESCO kuwa moja ya turathi za Ulimwengu.

Mwandishi: Shisia Wasilwa