1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wanne wa polisi wauawa Port-au-Prince

John Juma
1 Machi 2024

Makabiliano ya risasi kati ya polisi na magenge ya uhalifu katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, siku ya Alhamisi (Februari29) yalisababisha vifo vya maafisa wanne wa polisi.

https://p.dw.com/p/4d5N0
Maandamano nchini Haiti
Maandamano ya kumtaka Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry, ajiuzulu mjini Port-au-Prince.Picha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Kiongozi mashuhuri wa genge alisema mashambulizi yaliyoratibiwa na makundi yenye silaha yangeliendelea kwa lengo la kumtimua madarakani Waziri Mkuu Ariel Henry.

Milio ya risasi ilisikika katika jiji lote huku vikosi vya usalama vikipambana na washambuliaji waliokuwa wamelenga vituo vya polisi, vikiwemo viwili vilivyochomwa moto.

Maeneo mengine yaliyoshambuliwa namagenge hayo ni chuo cha polisi na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint-Louverture.

Soma zaidi: Mahakama Kenya yaizuwia serikali kupeleka askari Haiti

Afisa wa chama cha polisi aliliambia shirika la habari la AFP kuwa pamoja na maafisa wanne waliouawa, watano wengine walijeruhiwa.

Hayo yalijiri wakati Waziri Mkuu Henry akiwa nchini Kenya ambako nchi hizo mbili zilisaini makubaliano ya kujaribu kuokoa mpango wa taifa hilo la Afrika kupeleka polisi wake 1,000 nchini Haiti.

Kikosi hicho cha polisi ya kimataifa kilikusuiwa kuisaidia Haiti kupambana na magenge hayo yanayofanya uhalifu kwa viwango visivyo na kifani.