Loew: Hakujawahi kuwa na ubaguzi katika timu ya taifa
29 Agosti 2018Amefanyia mabadiliko kikosi kitakachoshiriki katika michezo ya kimataifa mwezi ujao, akisema, mlingano wa kuwa na uzoefu pamoja na vijana ni muhimu. Loew alisema leo (29.08.2018) kwamba Ujerumani, ambayo ilitolewa mapema katika kombe la dunia kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 80 katika awamu ya makundi, haikupaswa kucheza mchezo wao wa kawaida wa kumiliki mchezo katika mashindano hayo ya mtoano wakati timu zilikuwa zikifanya mashambulizi ya ghafla kwa mafanikio makubwa.
Pia amesema alishindwa kuingiza hali ya kuona umuhimu na hisia miongoni mwa wachezaji wake ambao walipoteza michezo yao miwili kati ya mitatu katika awamu ya makundi.
Miongoni mwa wachezaji aliowaita katika kikosi cha Ujerumani katika michezo ya ligi ya mataifa dhidi ya Ufaransa Septemba 6 na mchezo wa kirafiki dhidi ya Peru siku tatu baadaye, ni wachezaji wanaorejea katika kikosi hicho Leroy Sane, Nils Petersen na jonathan Tah pamoja na wageni Kai Havertz, ambaye ana umri wa miaka 19 , Thilo Kehrer , mwenye umri wa miaka 21, na Nico Shulz mwenye umri wa miaka 25.
"Uzoefu ni msingi muhimu hata kwa wanaoanza upya," Loew alisema. "Na wachezaji vijana, wenye uchu wanaweza kusaidia katika majukumu muhimu siku za usoni."
Mchezaji bora wa Premier League
Mshambuliaji wa pembeni Sane, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora kijana katika ligi ya England ya Premier League msimu uliopita baada ya kuisaidia Manchester City kupata ubingwa, Petersen na Tah waliondolewa kutoka katika kikosi cha mwisho kilichoshiriki katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwezi Juni.
Loew amemuacha mchezaji wa kati Sami Khedira, aliyekuwamo katika kikosi kilichoshinda kombe la dunia mwaka 2014, kwa ajili ya mechi za mwezi ujao lakini ameendelea kuwa na imani na wengine kadhaa ambao wamecheza chini ya kiwango nchini Urusi, miongoni mwa wachezaji 17 kati ya 23 waliokuwa katika kikosi kilichokwenda Urusi.
"Umiliki wa mpira katika ligi ni muhimu lakini katika awamu ya mtoano kunahaja ya kubadilika. Hilo lilikuwa kosa langu kubwa," Loew aliwaambia waandishi habari. "Kwamba naamini kwa mchezo wa kumiliki mpira tutapita katika awamu ya makundi.
"Nilitaka kufanya bora zaidi, na kufanya bora zaidi umiliki wa mchezo . Lakini kila mchezo ni wa mtoano. Nilipaswa kutambua kwamba tunahitaji kuchukua tahadhari zaidi. Badala yake nilitaka kuingia katika hatari zaidi."
Loew pia amesema alishindwa kuwatia hamasa zaidi wachezaji wake kwa ajili ya michuano hiyo.
"Baada ya kushinda mwaka 2014 na kuwa juu tulishindwa mara hii , kuwasha moto mkubwa ili kila mmoja ajihisi kuwa na hamasa," Loew alisema.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Idd Ssessanga