Libya kuwaondoa wawakilishi katika mazungumzo ya amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Libya kuwaondoa wawakilishi katika mazungumzo ya amani

Wajumbe wa serikali ya Libya inayotambulika kimataifa wamesema watawaondoa wawakilishi katika mazungumzo na waasi, wakilalamikia marekebisho yaliyofanywa katika rasimu yenye lengo la kumaliza mzozo nchini mwao.

Hali hii inaonesha kuwa ni mkwamo katika siku za hivi karibuni wa juhudi za umoja wa mataifa za kuhakikisha kuwa makubaliano yanafikiwa ifikapo Sept. 20 , mwaka huu kati ya serikali hiyo ya Libya na waasi.

Mataifa yenye ushawishi mkubwa ya magharibi yanasema lengo la Umoja wa mataifa la kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa ndio suluhisho pekee katika mgogoo huo ambao umeliweka katika hali mbaya ya kiuchumi taifa hilo la Afrika ya kaskazini ikiwa ni miaka minne tangu waasi wamuondoe kiongozi wa muda mrefu Muamar Gaddafi.

Serikali hiyo inayotambulika kimataifa na bunge lililochaguliwa wamekubaliana kuwa na makubaliano ya awali wakati upande huo uliojitenga bado umekataa kusaini makubaliano hayo wiki iliyopita katika mazungumzo yaliyofanyika katika mji wa Skhirat nchini Morocco.

U.N. yasema wajumbe wa serikali watarejea katika mazungumzo hayo

Bernadino Leon Mjumbe wa umoja wa mataifa katika mazungumzo ya upatanishi ya mzozo wa Libya

Bernadino Leon Mjumbe wa umoja wa mataifa katika mazungumzo ya upatanishi ya mzozo wa Libya

Mjumbe wa umoja wa mataifa katika mazungumzo hayo Bernardino Leon alisema ya kwamba pande zote mbili zilikuwa zimefikia muafaka na zilikuwa zinaelekea kutangaza wajumbe watakaounda serikali ya umoja wa kitaifa lakini hata hivyo wajumbe wa serikali katika mazungumzo hayo na wale wa bunge la wawakilishi wamesema ya kuwa wamewarejesha wajumbe wao kwa ajili ya kufanya mashauriano kuhusiana na mapendekezo hayo ya marekebisho katika rasimu hiyo.

Mjumbe mwingine wa bunge hilo pia alithibitisha kukataliwa kwa marekebisho yaliyoongezwa katika hatua hiyo ya mwisho ya mazungumzo lakini akasisitiza kuwa siyo rasimu yote.

Aidha mjumbe huyo alipuuza taarifa za kuwepo tofauti kati ya pande hizo mbili na kusema kuwa ni kawaida kuwepo kwa majadiliano ya aina hiyo hasa katika hatua za mwisho.

Aliongeza kuwa kuwa timu ya wajumbe wa bunge hilo linalotambulika kimataifa haitaondoka katika majadiliano hayo licha ya wito wa kurejea nchini Libya kwa ajili ya mashauriano zaidi. " Nadhani watarejea kesho au kesho kutwa na wataendelea na mazungumzo haya, aliongeza.

Mzozo huo nchini Libya unaonekana kuongeza kitisho kwa viongozi wa mataifa ya ulaya mnamo wakati wanamgambo wa kundi la dola la kiisilamu wakizidi kujiimarisha nchini humo huku wafanyabiashara wanaojihusisha na usafirishaji wahamiaji wakitumia mwanya wa mgogoro huo kusafirisha wahamiaji kupitia bahari ya Mediterania kwenda ulaya kwa njia zisizo halali.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/RTRE

Mhariri : Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com