1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen wawanyemelea Bayern kileleni

7 Desemba 2020

Kinyang'anyiro cha ubingwa wa Ujerumani kimekuwa kikali zaidi baada ya mabingwa Bayern Munich kulazimishwa sare ya 3-3 na RB Leipzig uwanjani Allianz Arena. Thomas Müller ni mshambuliaji wa Bayern Munich.

https://p.dw.com/p/3mKHy
FC Schalke 04 - Bayer Leverkusen
Picha: Guido Kirchner/dpa/picture alliance

"Tulifahamu kabla kuanza kwa mechi kwamba tukifungwa tunaweza kurudisha magoli na kurudi katika mechi. Kwamba kila mara tunaweza kurudi katika mchezo, hilo kwa bahati mbaya tumelifahamu leo tu. Lakini juu ya yote, la muhimu ni kwamba tumesalia vinara wa ligi. Kwa sasa tuna matatizo madogo tu lakini tutatazama ili tuhakikishe kwamba katika mechi ijayo tunaebuka na ushindi," alisema Müller.

Dortmund walazimishwa sare na Eintracht Frankfurt

Pointi hizo mbili walizozipoteza Bayern Munich zimewafanya Bayer Leverkusen kuupunguza mwanya na sasa tofauti iliyoko baina yao na miamba hao kutoka Bavaria ni pointi moja tu. Hii ni baada ya Leverkusen kupata ushindi wa tatu bila walipokuwa ugenini wakicheza na Schalke 04. Leverkusen wamewavuka RB Leipzig na Borussia Dortmund katika msimamo ila tofauti ya alama si kubwa.

Deutschland Frankfurt | Bundesliga | Eintracht Frankfurt v Borussia Dortmund
Youssouffa Mukoko wa Dortmund akabiliwa na Martin Hinteregger wa FrankfurtPicha: Alex Grimm/Getty Images

Baada ya FC Cologne kuwashangaza wiki mbili zilizopita hapo Jumamosi Dortmund walilazimishwa sare ya bao moja na Eintracht Frankfurt. Kocha wao Lucien Favre anasema bahati haikuwa upande wao ndiposa hawakutoa ushindi.

"Tunachukua pointi hii kwasababu ilikuwa ni moja bila katika kipindi cha kwanza ambapo Frankfurt walikuwa bora kutushinda. Katika kipindi cha pili tulijitahidi, tulikimbia sana na mpira badala ya kusimama. Kipindi cha pili kilikuwa kizuri zaidi na tungeweza kupata ushindi wa mbili kwa moja ila mwishowe mechi iliishia moja kwa moja. Na lazima tulikubali hilo," alisema Favre.

Kwa sasa Bayern Munich ndio wanaoongoza wakiwa na pointi ishirini na tatu Bayer Leverkusen wako pointi moja nyuma katika nafasi ya pili halafu RB Leipzig wanaishikilia nafasi ya tatu pointi zao zikiwa ishirini na moja na Borussia Dortmund wanawafuata katika nafasi ya nne na alama kumi na tisa.