1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kushner aendeleza kazi ya mkwewe Ulaya Mashariki

Zainab Aziz
4 Aprili 2024

Wakati Donald Trump akijiandaa kurejea Ikulu ya Marekani, mkwewe wa kiume, Jared Kushner, anaendeleza pale rais huyo wa zamani alipoishia katika biashara yenye kutiliwa shaka ya sekta ya ujenzi nchini Serbia na Albania.

https://p.dw.com/p/4eQI1
USA Donald Trump Jared Kushner
Jared Kushner (kushoto) akizungumza na mkwe wake, Donald Trump, wakati huo akiwa rais wa Marekani, Disemba 2021.Picha: Win McNamee/Getty Images

Miongoni mwa miradi ambayo Kushner anapanga kutekeleza ni kulijenga upya eneo kubwa katika mji mkuu wa Serbia, Belgrade.

Miaka miwili kabla ya Donald Trump kugombea urais mnamo mwaka 2016, aliwaambia viongozi wa Serbia kwamba alikuwa na lengo la kujenga hoteli ya kifahari na nyumba za kupangisha kwenye eneo ambalo hapo awali yalikuwa makao makuu ya jeshi la Yugoslavia ya zamani lililoharibiwa mnamo mwaka 1999 kwa kuripuliwa na majeshi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Hata hivyo, mradi huo ulishindikana. Lakini sasa Kushner, aliyekuwa afisa mwandamizi kwenye ikulu ya Marekani wakati wa utawala wa baba mkwe wake, amefikia makubaliano ya muda na serikali ya Serbia kuendeleza mradi huo.

Soma zaidi: Kushner akutana na Netanyahu na Abbas

Kulingana na gazeti la New York Times, makubaliano hayo ya miaka 99 bila malipo, yatamruhusu Kushner kujenga hoteli ya kifahari, majengo vya makaazi, maduka na jumba la kumbukumbu kwenye eneo husika.

Mtaji atakouhitaji kwa ajili ya mradi huo wa kiasi cha dola milioni 500 utatoka kwenye kampuni yake ya vitega uchumi aliyoianzisha baada ya kuondoka Ikulu.

Hana upungufu wa fedha

Kwa hakika mtaji anao wa kutosha. Tangu wakati huo inakadiriwa kwamba  ameweza kupata dola bilioni 2 kutoka kwenye mfuko wa vitega uchumi wa Saudi Arabia.

Trump ampa kazi ya ushauri mkwe wake

Wakati huo huo, kampuni za mitaji za Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar nazo pia zimemimina mamilioni ya fedha kwenye kampuni ya Kushner.

Hivi karibuni tu alisema kwamba pande zinazohusika na mradi huo zimekubaliana kimsingi kuikatia serikali ya Serbia mgao wa asilimia 22 wa faida itayotokana na mradi huo.

Soma zaidi: Kushner azuru Mashariki ya Kati

Rais Aleksandar Vucic wa Serbia alisema lazima serikali yake ilete maendeleo zaidi na kujenga fursa za biashara.

Milan Kovacevic, ambaye ni mtaalamu wa uchumi na mshauri wa uwekezaji, anaunga mkono haja ya kujenga uwezo mpya ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la watu, na ustawi wa sekta ya utalii kwenye jiji la Belgrade.

Mtaalamu huyo alisema jiji hilo linahitaji hoteli zaidi pamoja na zile zenye ubora wa viwango vya juu.

Utaratibu wakiukwa

Hata hivyo, mtaalamu huyo alikosowa taratibu zilizotumika katika kumpa zabuni mwekezaji mmoja tu, yaani Jared Kushner.

Alisema mchakato kama huo unaacha wazi mwanya mpana wa kufanyika ufisadi.

USA Jared Kushner Donald Trump
Mkwe wa Donald Trump, Jared Kushner, baada ya kuteuliwa kuwa mshauri mkuu wa Rais Trump mwaka 2020.Picha: Doug Mills/ Consolidated News Photos/picture alliance

Baadhi ya wanasiasa na wataalamu wa upinzani pia wanakerwa na mipango hiyo ya maendeleo wanayoiona kuwa ni kashfa inayopaswa kuzuiwa.

Kiongozi wa harakati za kutetea mazingira, Aleksandar Jovanovic Cuta, alisema mji wa Belgrade si mali binafsi ya Rais Vucic.

Soma zaidi: Rais wa Serbia adai ushindi wa chama chake katika uchaguzi wa Bunge kabla ya matokeo

Alieleza kwamba hayo yanatokea pia katika maliasili za Serbia: mito, misitu na madini.

Mwanaharakati huyo  alisema rais waSerbia anagawa kila kitu cha thamani bila ya kuwafahamisha wananchi juu ya mikataba inayofikiwa iwapo inawanufaisha wananchi hao.

Aliyekuwa mhandisi mkuu wa ujenzi katika mji wa Belgrade miaka kadhaa iliyopita, Dorde Bobic, alisema amekasirishwa juu ya miradi inayopangwa kutekelezwa.

"Miradi hii inaonesha kiburi cha hali ya juu. Inawezekana vipi kumpa kandarasi mtu anayetoka nchi iliyoupiga mabomu mji wa Belgrade mnamo mwaka wa 1999?" Anauliza.