1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kupanda na kushuka kwa uchumi wa Kenya

10 Desemba 2013

Kenya ni kituo kikuu cha masuala ya biashara na fedha katika eneo la Afrika ya Mashariki na mlango wa kuingilia kwenye eneo hilo, ikiwa na uchumi uliojikita kwenye soko unaoongozwa kwa sera ya kiliberali.

https://p.dw.com/p/1AW3X
Tembo kwenye mbuga za Kenya, moja ya vivutio vya utalii.
Tembo kwenye mbuga za Kenya, moja ya vivutio vya utalii.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Miaka 50 ya uhuru wa Kenya, imeshuhudia uchumi wa taifa hilo la Afrika ya Mashariki ukipanda na kushuka tangu mwaka 1963.

Katika miaka ya mwanzoni mwa uhuru, nchi hiyo ilifikia ukuwaji wa asilimia 6 ya ukuwaji wa uchumi, ambayo katika miongo kadhaa iliyofuatia hapo ikaanguka hadi asilimia 4.

Katika miaka 1990, pato la jumla la uchumi wa Kenya lilijikuta likikabiliwa na kiwango kikubwa cha kuyumba, kikiwa baina ya chini ya asilimia 4 na 4, lakini kikapanda hadi kufikia asilimia 7 mwaka 2007.

Ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2008, pamoja na athari za mtikisiko wa uchumi duniani kwa fedha zinazotumwa nyumbani na Wakenya walio nje na pia usafirishaji nje ya nchi, kulishusha ukuwaji wa pato jumla la Kenya hadi asilimia 1.7, lakini katika mwaka 2010-11, uchumi huo ukaja tena juu hadi asilimia 5, huku matarajio kwa miaka ijayo yakiwa mazuri.

Ikiwa hali itaendelea kama ilivyo sasa, Kenya inatazamiwa kuwa nchi ya kwanza ya Afrika ya Mashariki kutoka kwenye hadhi ya pato la chini na kuwa ya pato la kati. Pato la jumla la sasa kwa mtu ni dola 760 kwa mtu kwa mwaka.

Gharama za maisha

Hata hivyo, kupanda kwa gharama za maisha, ambako kumefikia hadi asilimia 12, kumekuwa tatizo kwa miaka kadhaa sasa, ingawa sera kali za kifedha zinasadia kupunguza kushuka kwa thamani ya fedha na matarajio ni kwamba bei za bidhaa muhimu zitarudishwa kwenye tarakimu moja hivi karibuni. Sarafu ya shilingi ya Kenya imetulia sasa baada ya kuporomoka vibaya katikati ya mwaka 2011.

Mlima Kenya.
Mlima Kenya.Picha: AFP/Getty Images

Inaaminika kwamba juhudi endelevu za kuongeza usafirishaji bidhaa nje na uwekezaji kwenye miundombinu ya usafiri na nishati kutasaidia kuongeza kasi ya ukuwaji wa uchumi na kuimarisha nafasi ya Kenya kimataifa.

Kwa upande wa viwanda, Kenya inatambuliwa kama nchi ya kiviwanda zaidi kwenye eneo la Afrika ya Mashariki na Kati.

Washirika wakuu wa usafirishaji kwa Kenya ni pamoja na mataifa mengine yote ya Afrika ya Mashariki na pia Uingereza, Uholanzi na Marekani. Waingizaji wakuu wa bidhaa nchini humo ni pamoja na China, India, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Afrika ya Kusini.

Miongoni mwa viwanda maarufu nchini Kenya ni vile vinavyozalisha bidhaa ndogo ndogo za matumizi ya nyumbani pamoja na vya kusindikia vyakula.

Kilimo kimekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya kwa miaka kadhaa na nchi hyo imekuwa chanzo cha bidhaa nyingi za kilimo kwa ajili ya usafirishaji nje ya nchi. Sekta hiyo imesambaa vyema takribani nchini kote, huku maeneo mbali mbali yakipendelea kuzalisha aina tafauti ya mazao ya kilimo na mengine kulingana na hali za hewa za maeneo husika.

Utalii pia ni sekta nyengine kuu ya uchumi wa Kenya, ambapo kwa kutambua umuhimu wake, awamu mbalimbali za serikali zimekuwa zikielekeza jitihada zake sana kwenye kuinua biashara ya utalii na kuwavutia watalii na wageni duniani kote.

Katika siku za karibuni, sekta ya nishati imepata msukumo mkubwa baada ya ugunduzi wa kiwango kikubwa cha mafuta, gesi na joto la ardhini katika maeneo mbalimbali ya Kenya. Ugunduzi huu unatarajiwa kuubadilisha kabisa uchumi wa Kenya kwa kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa nishati kwenye njia zake kuu za uchumi.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Chanzo: The Economist