Kenya yaadhimisha miaka 50 ya uhuru wake | Miaka 50 Uhuru wa Kenya | DW | 10.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Miaka 50 ya Uhuru Kenya

Kenya yaadhimisha miaka 50 ya uhuru wake

Tarehe 12 Desemba 1963, Kenya ilipata uhuru wake kutoka Uingereza na bendera ya mkoloni, maarufu kama Union Jack, ikashushwa na bendera ya rangi nyeusi, nyekundu na kijani ikapandishwa kuashiria uzao wa taifa jipya.

Siku ya uhuru wa Kenya tarehe 12 Disemba 1963.

Siku ya uhuru wa Kenya tarehe 12 Disemba 1963.

Kutoka utawala wa Wazungu 55,759, sasa nguvu za madaraka zikaangukia kwenye mikono ya Waafrika 8,365,942, kwa mujibu wa gazeti la The New York Times.

Safari ya kuelekea kwenye uhuru ilianza kwenye miaka ya 1950 kwa uasi wa Mau Mau, vuguvugu la wanamgambo wa Kiafrika waliopingana na utawala wa kikoloni na unyonyaji wake dhidi ya wenyeji.

Wapiganaji wa vuguvugu hilo, ambao wengi wao walikuwa kutoka kabila kubwa la Kikuyu, waliwashambulia viongozi wa kikoloni na walowezi. Mwaka 1952, serikali ya kikoloni ikatangaza hali ya hatari na kuwakamata viongozi wengi wa kupigania uhuru nchini Kenya, wakiwemo hata wale wenye msimamo wa wastani na au wasio na mahusiano yoyote na Mau Mau, kama vile Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa chama cha Kenya African Union (KAA), ambacho baadaye kikaja kuwa Kenya African National Union (KANU).

Kushindwa kwa Mau Mau

Mzee Gitu wa Kahengeri, msemaji wa wapiganaji wa zamani wa Mau Mau.

Mzee Gitu wa Kahengeri, msemaji wa wapiganaji wa zamani wa Mau Mau.

Kati ya mwaka 1952 hadi 1956, utawala wa Kiingereza uliwashinda wapiganaji wa Mau Mau kutokana na kampeni kali na ya kikatili ya kijeshi na kuwakamata maelfu ya watu wa kabila la Kikuyu. Lakini kufika wakati huo, uasi wa Mau Mau ulikuwa umeshauonesha utawala wa kikoloni kwamba kulihitajika mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa na kilimo.

Mwaka 1957, utawala huo ukaruhusu uchaguzi wa kwanza wa moja kwa moja wa Baraza la Kutunga Sheria na kufikia mwaka 1960 Waafrika wakawa ndio wengi kwenye Baraza hilo.

Kwa miaka mingine kadhaa baadaye, utawala wa kikoloni ukalazimika kufanya kazi pamoja na viongozi wa Waafrika na wawakilishi wa walowezi kupanga kipindi cha mpito kuelekea uhuru wa nchi hiyo.

Makongamano hayo yakazaa katiba ya mwaka 1963, ambayo ilitoa muongozo wa uchaguzi uliofanyika Mei. KANU ilipata wingi wa viti kwenye mabaraza yote mawili ya bunge na kumchagua kiongozi wake, Kenyatta, ambaye alikuwa ametolewa jela mwaka 1961, kuwa waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo jipya, kukiwa na matumaini mapya kutoka kwa umma wa wananchi wa Kenya.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Chanzo: The New York Times

DW inapendekeza