1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kupanda miti kutapunguza mabadiliko ya tabia nchi; Utafiti

Sekione Kitojo
5 Julai 2019

Njia bora zaidi  ya  kupambana  na  ongezeko la ujoto  duniani  ni kupanda  miti  mingi,kadiri iwezekanavyo, kwa  mujibu  wa utafiti uliotolewa na mwanasayansi  mmoja  wa Uswisi.

https://p.dw.com/p/3Lck8
Paris Klimaproteste
Picha: Reuters/C. Platiau

Mwanasayansi huyo  anasema  katika  utafiti  wake  kuwa tunahitajika  kupanda takriban  miti trilioni moja, ama  huenda  zaidi. 

Habari nzuri ni  kwamba  tunaweza  kusaidia  kuzuwia  mabadiliko  ya tabia  nchi  kwa  kufanya  kampeni  kabambe ya  kupanda  miti, kwa mujibu  wa  utafiti  mpya  uliochapishwa  jana Alhamis. Lakini  kuna habari  mbaya  pia,  kwa sababu tunahitajika  kupanda miti  katika eneo linalofikia  ukubwa  wa  nchi  kama  Marekani  ama  nusu  hivi ya  bara  la  Afrika, na  hata  hivyo  baadhi  ya  wanasayansi wanatia  shaka  juu  ya  hitimisho  la  utafiti  wa  waraka  huo.

Kenia "Mount Kenya"
Misitu inaweza kuhifadhi gesi nyingi ya kaboni Picha: AFP/T. Karumba

Juhudi  kama  hizo  zitaweza  kuhifadhi  theluthi  mbili  ya  gesi  za kaboni  zinazotolewa  na  binadamu  na  kupunguza  viwango  vya jumla  katika  anga  hadi  katika  kiwango  cha  chini  katika  karibu karne moja, kwa  mujibu wa  utafiti  ambao  ulifanywa na  ETH Zurich na  kuchapishwa  katika  jarida  la  sayansi.

Utafiti  huo  ni  wa  kwanza  kujaribu  kuelezea  ni miti  mingapi  dunia inaweza kusaidia  dunia, wapi  pa  kupandwa  miti  hiyo na  ni  kiasi gani  cha  kaboni  kinaweza  kuhifadhiwa  na  miti  hiyo.

Brasilien Forschung Wissenschaft Sensoren Klima Temperatur Regenwald
Misitu ni muhimu kufyonza gesi chafu za kaboni zinazohifadhi joto anganiPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Giusti

Nafasi ya kupanda miti

Na  kuna  nafasi  ya  kutosha, anasema  mtafiti  huyo mwanasayansi  kutoka  Uswisi. Hata kwa  kuwa  na  miji  iliyopo hivi sasa na  eneo  la  mashamba, kuna  nafasi  ya   kutosha  kupandwa miti  mipya  kuweza  kuenea  katika  kilometa  za  mraba  milioni 9. Eneo  hilo  ni takriban  eneo  sawa  na  Marekani.

Utafiti  huo  umepiga hesabu  kwamba  kwa  muda  wa  miongo kadhaa, miti  hiyo  mipya  inaweza  kufyonza  karibu  tani  za  ujazo milioni 830 za gesi  ya  kaboni dioxide  ambayo  huhifadhi joto kutoka  katika  anga. Hii  ni  kiasi  ya uchafuzi mkubwa wa  kaboni kama  ilivyotolewa  na  binadamu  katika  kipindi  cha  miaka  25 iliyopita.

India Chhattisgarh
Miti katika wilaya ya Chhattisgarth , India Picha: Imago/Hindustan Times

Manufaa  makubwa yatakuja  haraka  kwasababu  miti inaondoa kaboni  zaidi  kutoka  katika  hewa  wakati  ikiwa  michanga, waandishi  wa  utafiti  huo  wanasema.

Uwezekano  wa  kuondoa  kaboni  nyingi  zaidi  uko  katika  maeneo ya  tropiki.

Mataifa  sita  ambayo  yana  nafasi  kubwa  kwa kupanda  miti mipya  ni  Urusi , Marekani, Canada, Australia , Brazil  na  China.