Kumbukumbu ya miaka 32 ya mauaji ya kimbari Rwanda
7 Aprili 2026
Shughuli za kumbukumbu hizi zimeanzia mapema leo katika jumba la kumbukumbu ya mauaji hayo lililoko mjini Kigali ambako kumezikwa waathiriwa wa mauaji hayo zaidi laki mbili na nusu. Miongoni mwa waliohudnuria ni viongozi wakuu wa serikali, manusura wa mauaji hayo, na wanadiplomasia wa nchi za kigeni.
Ni zoezi ambalo pia limeshuhudia hisia kali za ushuhuda kutoka kwa manusura hasa jinsi namna walivyoponea chupuchupu mauaji hayo. Mmoja wao ni Ngiruwonsanga akizungumza kwa urefu akifafanua maajabu yaliyompata hadi akanusurika kama hatua ya kuonyesha ukali wa mauaji hayo yaliyofanyika kwa siku mia moja ambapo watu zaidi milioni moja walipoteza masiah yao.
"Interahamwe walinikamata baada ya kuwa nimejificha katika idadi kubwa ya maiti waliouawa,waliponikamata walimwambia mmpja wa watoto wadogo ambao nilikuwa nikisoma nao shule moja kabla ya mauaji, alikuwa na mkuki wakamwambia aniongoze hadi katika eneo la karibu ambapo kulikusanyika watu wengi kwa ajili ya kuuawa, tulipofika pale, yule kijana ni kama alizubaa kidogo akiwatazama wa-interahamwe waliokuwa wakiuawa mimi baada ya kuona amezubaa kidogo nilikimbia."
Ushuhuda mwingine ulitolewa na viongozi pamoja na manusura wengine umejikita juu ya namna gani mataifa ya kigeni hasa Ufaransa na Ubelgiji yalivyopandikiza mbegu ya ukabila na chuki hadi kusababisha wanyarwanda kuuana wao kwa wao.
Rais Paul Kagame ambaye alizungumza kwa sauti iliyojaa hisia amezungumza kwa lugha ya Kinyarwanda lakini baadaye akabadili kwa lugha ya kiingereza kama ishara ya kutaka ujumbe wake ufike kwa walengwa. Hii ikizingatiwa kuwa ni wiki chache tu baada ya serikali ya Marekani kuliwekea vikwazo jeshi la Rwanda kwa tuhuma za kulisaidia kundi la M23 linalopambana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Hakuna vikwazo au kejeli kutoka nje ambazo zinaweza kuchafua heshima na hekima ya vikosi vya ulinzi na usalama vya Rwanda, ambavyo ni miongoni mwa vikosi bora kabisa vinavyoweza kupatikana mahala popote, natazamia kuibua hoja hii ya vikwazo katika ngazi ya kimataifa, ili kuweza kuelewa hasa kiini na mazingira ya uonevu huu."
Rais Kagame amesema, mauaji ya namna hii hayawezi kutokea tena nchini Rwanda licha ya kwamba kwa kauli yake itikadi ya ukabila na ubaguzi inaendelea kuota mizizi katika eneo la maziwa makuu lakini kwamba hilo haliwezi kutokea tena Rwanda, amesema kuwa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa umekuwa ngome kubwa ya wapinzani wa serikali ya Kigali huku akitoa mfano wa mikutano inayoendelea mjini Kinshasa ambayo inamhusisha Jean Luc Habyarimana ambaye ni mtoto wa Rais wa zamani wa Rwanda Juvenali Habyarimana.
Kagame amewapuuza wapinzani hao na kusema misaada wanayopewa na Kinshasa ni kelele tupu. Huku akiendelea kusema kuwa usalama unaopatikana Rwanda leo ni matokeo ya jeshi ambalo limejengwa kwa misingi ya kihistoria
"Utamaduni na mienendo ya jeshi letu hii RDF ilijengwa kwa kuzingatia nyakati ngumu tulizozipitia, haya yana pia ni miongozo ya majeshi yetu yanayofanya kazi katika michakato ya kuleta amani katika nchi za kigeni ambapo limejipatia heshima ya kimataifa."
Maadhimisho haya yanafanyika wakati eneo la maziwa makuu likikabiliwa na vita hasa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambavyo wachambuzi wanahisi kwa kiasi kikubwa vinasababishwa na itikadi ya ukabila isiyoisha. Kwa mara ya kwanza shughuli za kumbukumbu hizi zimefanyika bila kupewa uzito kama ilivyokuwa hapo awali, wakati huu kwa muda wa wiki nzima wa kumbukumbu hii, wananchi wataruhusiwa kuendelea na shughuli zao tofauti na ilivyokuwa hapo awali.