1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuacha madaraka kwa Kansela Schröder

Ramadhan Ali13 Oktoba 2005

Uamuzi wa Kansela Schröder kuondoka madarakani ni mada mkuu wa magazeti ya Ujerumani ya hii leo.

https://p.dw.com/p/CHMZ

Kuhusu uamuzi wa Kanzela Schröder kutojiunga na serikali mpya ya muungano wa vyama vikuu, gazeti la OFFENBURGER TAGEBLATT laandika:

“Kuondoka jukwaa la kisiasa kwa Kansela Gerhard Schröder, kuna maana chama cha SPD kimeshindwa kabisa katika uchaguzi wa Septemba 18.Bila ya Schröder chama cha SPD kingejikuta tabuni kuweza kutamba katika serikali ya muungano na chama cha CDU/CSU na kujiandaa kwa uchaguzi ujao.Kwani, kwa kun’gatuka Schröder chama cha SPD kinapoteza kiongozi wake mwenye busara,mkakati, mwerevu na ajuwae kupambana na wapinzani wake wa kisiasa.”

Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE linalochapishwa Potsdam laandika:

„Schröder bila kuchelewa amebainisha wazi kwamba dai lake la kuungan’gania wadhifa wa ukanzela lilikua turufu tu katika meza ya majadiliano.Mafanikio ya turufu hiyo alioicheza,yafaa kushangiriwa. Viwanja vyote vya kufanyiwa mageuzi miaka ijayo- kuanzia bajeti ya serikali, bima za afya hadi soko la kazi mpaka bima ya uzeeni viko chini ya dhamana za mawaziri wa chama cha SPD. Na nani alietarajia hayo miezi michache nyuma pale chama cha SPD kilipoanza kukaribia kusambaratika kama chama kikubwa cha umma ?-"lauliza gazeti.

Gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG laandika kwa hasira:

„Gerhard Schröder amekiacha kiti chake kitupu-swali sasa kikaliwe na nani ?

Wanasiasa werevu wa Social democratic party hawajitokezi safu ya mbele hadi sasa.Akiondoka mmojawao madarakani, chama chochote hufaidika kukaribisha upepo mpya na mkondo mpya wa kisiasa. Lakini, chini ya shinikizo la kuwamo katika serikali ya muungano wa vyama vikuu,chama cha SPD hakitadiriki kukaribisha upepo na mkondo huo. Kinyan’ganyiro cha kuania mageuzi ya mkondo wa kisiasa kwa siku zijazo ambacho kimeshaanza wazi hivi sasa,hakitoa dalili njema kwa utulivu wa serikali ijayo."

Gazeti la ABENDZEITUNG linalochapishwa Munich laandika kwamba, "kumsaka mtu gani angejaza nafasi ya Schröder kama makamo wa Kanzela chama cha SPD kimedharau kutafuta na mapema mrithi wa Schröder. Kati ya vigogo vya zamani kama waziri wa ulinzi Struck, waziri wa ndani Schily na msichana - chipukizi Nahles kuna mwanya mkubwa. Mbali na swali zima la viongozi,wakati umewadia kwa vyama vya CDU/CSU na SPD kuanza majadiliano yao ya kuunda serikali", lasisitiza ABENDZEITUNG kutoka Munich.

Likitugeuzia mada, gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linatuchukua katika mkasa wa wakimbizi wa kiafrika na sera ya Umoja wa Ulaya juu yake:

"Afrika kabisa si kisa cha kushughulikiwa na ‚mawaziri wa ulinzi’ bali ni mada ya mawaziri wa nje na wa misaada ya maendeleo. Bila shaka, wakimbizi watakuja Ulaya kwa kadri chanzo halisi cha wakimbizi hakijatatuliwa - nacho ni ufukara pamoja na mwanya wa tofauti za hali ya kimaisha kati ya bara la Ulaya na jirani yake Afrika.

Ikiwa Umoja wa Ulaya utatia maanani ipasavyo jukumu lake la kuisaidia Afrika, ukitaka kupigiwa mfano na kuhifadhi hadhi zake zakutetea haki za binadamu, mkakati wake unapaswa kufanya yote 2 wakati mmoja:kulisaidia bara la Afrika, kutunga sera moja ya kukabiliana na wakimbizi na kuruhusu uhamiaji kihalali katika nchi za Ulaya.“