1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kolo Muani ajaza pengo la Nkunku Qatar

Josephat Charo
16 Novemba 2022

Mshambuliaji wa klabu ya Bundesliga Eintracht Frankfurt Randal Kolo Muani amejaza pengo la mshambuliaji wa RB Leipzig Christopher Nkunku katika timu ya taifa ya Ufaransa katika kombe la dunia Qatar 2022.

https://p.dw.com/p/4JbDy
Champions League Sporting Lissabon vs Eintracht Frankfurt
Picha: Carlos Costa/AFP/Getty Images

Mabingwa watetezi Ufaransa wamekuwa na mkosi mbaya wa majeruhi kuelekea mashindao hayo. N'Golo Kanté, Paul Pogba na Presnel Kimpembe hawakujumuishwa kikosini na sasa Nkunku amejeruhiwa kwenye goti wakati wa mazoezi alipokabiliana na Eduardo Camavinga. Ufaransa imesema katika twita kwamba timu nzima imehuzunika pamoja na Nkunku na inamtakia apone haraka.

Kolo Muani mwenye umri wa miaka 23 amefunga mabao matano katika Bundesligamsimu huu wa sitini na anaongoza katika orodha ya wachezaji waliotoa pasi zilizosaidia mabao kutiwa kambani, akiwa ametoa jumla ya pasi tisa kufikia sasa. Nkunku anaongoza orodha ya ufungaji magoli akiwa na jumla ya mabao 12.

Taarifa ya Ufaransa imesema Kolo Muani raia wa Ufaransa mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sasa yuko Japan na klabu yake Eintracht Frankfurt na atawasili Doha siku ya Jumanne wiki ijayo. Ufaransa itaanza kampeni ya kulitetea kombe la dunia Jumanne Novemba 22 itakapokwaana na Australia. Pia itakuwa na miadi na Denmark na Tunisia katika mechi za kundi D. 

Akizungumzia pambano lao dhidi ya Ufaransa mshambuliaji wa Australia Craig Goodwin alisema, "Bila shaka tutausoma mchezo na mfumo wao na kuangalia mbinu wanazotumia kuwa wakali uwanjani na jinsi tunavyoweza kuwaumiza. Nadhani tunafahamu Ufaransa ni timu kali na haiwezekani kupata mechi rahisi katika kombe la dunia. Tuna shauku kubwa na tutacheza bila presha kwa sababu sisi ni timu yenye uwezo mdogo kuliko Ufaransa na nadhani tunajiamini."

Beki wa Ufaransa, Axel Disasi alikuwa tayari amejaza nafasi ya beki Kimpembe tangu kikosi kilipotajwa wiki iliyopita. Beki mwenzake Raphael Verane anashiriki mashindano hayo akiwa na jeraha.

Fussball I RB Leipzig - SC Freiburg I Christopher Nkunku
Christopher NkunkuPicha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance

Mshambuliaji wa klabu ya Bundesliga Borussia Moenchengladbach Marcus Thuram alijumuishwa dakika za mwisho katika kikosi cha Ufaransa, huku kocha Didier Deschamps akitaja mara ya kwanza kikosi cha wachezaji 25 akibakisha nafasi moja kukamilisha kikosi cha wachezaji 26.

Orodha ndefu ya wachezaji nyota wanakosa mashindano ya kombe la dunia Qatar au wanauguza majeraha, huku baadhi ya wachambuzi wa soka wakijiuliza ikiwa ratiba kupangwa Novemba na Desemba kumechangia, ikizingatiwa wachezaji wamekuwa na kibarua kipevu cha kucheza katika msimu ulioshehehi shughuli nyingi.

Timu zaanza kuwasili Doha

Timu ya Ufaransa inatarajiwa kuwasili leo mjini Doha, ikipania kuwa timu ya kwanza kulitetea kombe la dunia tangu Brazil ilipofanikiwa kufanya hivyo 1962. Wachezaji kumi kati ya timu iliyoshinda kombe la dunia nchini Urusi 2918 wamo kikosini, akiwemo nahodha Hugo Lloris, Kylian Mbappe na Antoine Griezmann. Mshindiw a Ballon d'Or Karim Benzema, abmaye alikosa mechi kadhaa na klabu yake Real Madrid msimu huu kwa sababu ya jeraha, anajiandaa kwa kombe lake la kwanza la dunia tangu 2014.

Timu ya Argentina inatarajiwa pia kuwasili hivi leo Doha. Argentina inaanza michuano na Saudi Arabia Novemba 22, na baadaye itakabna koo na Mexico na Poland katika kundi C. Kocha wa Argentina Lionel Scaloni amesema amejaribu kuounguza shinikizo kwa timu yake, akisema wanafahamu soka linawakilisha nini kwa Argentina lakini ni mchezo na ndio maana wanatakiwa watie bidii uwanjani na wacheze mchezo wao.

England na Uholanzi zilikuwa nchi za kwanza zenye uwezo mkubwa kutoka Ulaya kuwasili Doha jana Jumanne. Mashabiki wa England kutoka India ni wengi zaidi kuliko mashabiki kutoka England, wakati kikosi hicho cha kocha wa England Gareth Southgate kilipokuwa kikielekea katika kambi yao.

(dpa,afp)