Kocha wa Ujerumani Löw arefusha mkataba | Michezo | DW | 18.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kocha wa Ujerumani Löw arefusha mkataba

Timu ya soka ya Ujerumani tayari imejikatia tikiti ya kushiriki katika fainali ya dimba la Kombe la Dunia nchini Brazil, na ilifuzu bila kushindwa mechi hata moja chini ya Uongozi wa kocha Joachim Löw

Kikosi cha Ujerumani ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kutamba nchini Brazil, na kocha Joachim Löw atasalia kuwaongoza vijana hao hadi Julai mwaka wa 2016 baada ya mkataba wake kurefushwa kwa miaka mingine miwili.

Löw mwenye umri wa miaka 53, ambaye mkataba wake wa sasa unakamilika mwaka wa 2014 baada ya Kombe la Dunia, alichukua usukani baada ya dimba la mwaka wa 2006, na tangu wakati huo, akaiongoza Ujerumani hadi fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka 2008 na kisha nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010 na Euro 2012.

Andre Schürrle akiifungia timu yake ya Ujerumani goli la tatu dhidi ya Sweden katika ushindi wa 5-3

Andre Schürrle akiifungia timu yake ya Ujerumani goli la tatu dhidi ya Sweden katika ushindi wa 5-3

Ubelgiji, Colombia na Uswisi, ni timu tatu zitakazowekwa katika makundi ya timu bora kwa mujibu wa orodha ya FIFA. FIFA imeamua kuwa timu saba bora katika orodha ya kimataifa zitapangwa pamoja na wenyeji Brazil.

Viongozi wa muda mrefu Uhispania, ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, bado wako kileleni, wakifuatwa na Ujerumani na Argentina. Colombia na Ubelgiji wanafuata licha ya kutocheza katika kombe la dunia la mwaka wa 2010. Uruguay waliofika katika nusu finali mwaka wa 2010 wako katika nafasi ya sita lakini ni lazima wawashinde nambari 70 Jordan katika mechi ya mchujo ya mikondo miwili mwezi ujao ili kufuzu katika droo ya kombe la dunia itakyoandaliwa mnamo Desemba 6 mjini Salvador. Uswisi ni ya saba, wakati Uholanzi ikifunga orodha ya timu nane bora.

Jumla ya timu 21 tayari zimejikatia tikiti ya kombe la dunia, huku nyingine 22 zikisubiri kujua hatma yao ili kuwapata washindi 11 baada ya mechi za mchujo. Timu zilizofuzu ni, wenyeji, Brazil, Japan, Australia, Iran, Korea Kusini, Uholanzi, Italia, Marekani, Costa Rica, Argentina, Ubelgiji, Uswisi, Ujerumani, Colombia, Urusi, Bosnia-Hercegovina, England, Uhispania, Chile, Ecuador, Honduras.

Zile ambazo bado ziko katika harakati ya kupata kibali ni, Ugiriki, Ufaransa, Ureno, Ukraine, Sweden, Iceland, Romania, Croatia, New Zealand, Mexico, Jordan, Uruguay, Cote d'Ivoire, Senegal, Ethiopia, Nigeria, Tunisia, Cameroon, Ghana, Misri, Burkina Faso na Algeria.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters

Mhariri: Yusuf Saumu