1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Tunisia Ghannouchi aanza mgomo wa kula

Bruce Amani
20 Februari 2024

Kiongozi wa upinzani wa Tunisia Rached Ghannouchi ameanza jana mgomo wa kula gerezani, na kujiunga na wakosoaji wengine wa serikali wanaogoma kupinga kile wanachokiona kuwa ni kufungwa jela bila haki

https://p.dw.com/p/4cb1L
Kiongozi wa Ennahda Rached Ghannouchi
Chama cha upinzani Tunisia Ennahda kinapinga ukandamizaji unaofanywa na Rais Kais SaiedPicha: FETHI BELAID/AFP

Kiongozi wa upinzani wa Tunisia Rached Ghannouchi ameanza jana mgomo wa kula gerezani, na kujiunga na wakosoaji wengine wa serikali wanaogoma kupinga kile wanachokiona kuwa ni kufungwa jela bila haki. Imed Khemiri, msemaji wa chama chake cha kisiasa, ameliambia shirika la habari la AP kuwa mgomo wa Ghannouchi unanuia kuonyesha masaibu ya wafungwa wa kisiasa wa Tunisia na ukiukaji wa uhuru wao.

Ghannouchi mwenye umri wa miaka 82,ni muanzilishi mwenza na mkuu wa chama cha Ennahda, kilichoingia madarakani Tunisia baada ya nchi hiyo kumuangusha aliyekuwa rais Zine el-Abidine Ben Ali mwaka wa 2011.

Alifungwa jela miaka mitatu mapema mwezi huu kwa mashitaka yanayohusiana na ufadhili wa kigeni wa kampeni za kisiasa za Ennahda mwaka wa 2019. Wakosoaji wengine sita wa Rais Kais Saied waliofungwa jela tangu Februari 23 kama sehemu ya uchunguzi kuhusu njama ya kuvuruga usalama wa taifa walianza mgomo wa kula wiki iliyopita.

Polisi mwaka huu wamewakamata vigogo kadhaa wa kisiasa ambao wanamtuhumu Saied kwa mapinduzi kufuatia hatua zake za kulivunja bunge na kuongoza kwa amri za rais kabla ya kuiandika upya katiba. Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 81 alikuwa spika wa bunge lililochaguliwa, ambalo lilivunjwa na Saied mwaka wa 2021 wakati alipojilimbikizia madaraka yote.