1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kijeshi Sudan ajiteua tena kuongoza serikali

Lilian Mtono
12 Novemba 2021

Jenerali mwandamizi aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi hivi karibuni nchini Sudan Abdel-Fattah Burhan amejiteua tena kuongoza baraza tawala la mpito ikiwa ni hatua inayoashiria nia yake ya kuimarisha udhibiti madarakani.

https://p.dw.com/p/42uXP
Putsch im Sudan | General Abdel Fattah al-Burhan
Picha: /AP/dpa/picture alliance

Wengi wa walioteuliwa ni watawala waliokuwa kwenye baraza lililopita. 

Hatua hii inachukuliwa katikati ya ahadi zinazotolewa kila mara na watawala wa kijeshi kwamba watarejesha mamlaka kwa serikali ya kiraia, tangu mapinduzi ya Oktoba 25 ambayo yalifuatiwa na maandamano makubwa ya wanaounga mkono demokrasia wanaoshinikiza kurejeshwa kwa utawala huo wa kiraia.

Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo ambaye ni mshirika wa karibu wa Burhan ametajwa kuwa makamu wa rais, pamoja na majenerali wengine watatu waliorejeshwa. Viongozi watatu wa makundi ya waasi waliopigana vita upande wa Omar al-Bashir pia wamejumuishwa kwenye baraza hilo lenye wajumbe 11 na wawakilishi watano toka upande wa kiraia.

Mohammed Hamdan Dagalo
Jenerali na mshirika wa karibu wa Burhan Mohammed Hamdan Dagalo amerejeshwa kwenye baraza hilo kama makamu wa rais.Picha: picture-alliance/AP Photo

Soma Zaidi: Waziri mkuu wa Sudan kurejea madarakani? 

Miongoni mwa wajumbe watano wa kiraia waliorejeshwa ni Raja Nicola ambaye ni mwanasheria na miongoni mwa wanawake wawili walioteuliwa.

Malik Agar, kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa kundi la waasi la Sudan Revorutionary Front lililojitika katika jimbo la Blue Nile kusini mwa taifa hilo ni miongoni mwa viongozi hao wa waasi aliyejumuishwa kwenye baraza hilo ambaye mwaka 2020 alikubali kusaini makubaliano ya amani ya kihistoria na serikali ya mpito ya mjini Juba nchini Sudan Kusini.

Lakini uteuzi huo tayari umekabiliwa na ukosoaji. Kwanza muundo wake unakosolewa kwa kushindwa kukidhi vigezo muhimu vya kuhusisha makundi makuu ya wanaodai demokrasia na kundi kubwa lililoongoza vuguvugu lililomuondoa al-Bashir la Declaration of Freedom and Change limesema litapinga hatua hiyo ya jenerali Burhan kujiteua tena kuongoza baraza hilo.

Waziri wa habari na utamaduni wa Sudan Hamza Baloul aliyekuwa akizuiwa kuzuizini wakati kulipofanyika mapinduzi hayo na baadaye kuachiwa, amekosoa uteuzi huo akiutaja kama hatua tu ya kuendeleza mapinduzi na kuongeza kuwa waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wana haki ya kukataa makubaliano na viongozi wa kijeshi.

Sudan | Massenproteste gegen Militärputsch in Omdourman
Waandamanaji wanaotaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia wanatarajiwa kuingia upya mitaani kupinga uteuzi huo mpyaPicha: AFP/Getty Images

Waandamanaji hao pamoja na kupinga mikakati inayoungwa mkono kimataifa ya kuwataka kurejea kwenye makubaliano ya kushirikishana madaraka na jeshi pia wameitisha mgomo wa nchi nzima.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric kwa upande wake amesema wanaifuatilia hatua hiyo iliyofikiwa nchini Sudan ambayo wameitaja kuwa ni ya kutia wasiwasi. Amesema wanataka kuona serikali ya kiraia inarejea haraka iwezekanavyo pamoja na kuchiwa kwa viongozi wa kisiasa wanaozuiwa.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes hapo jana aliliarifu baraza la Usalama la Umoja huo kwenye kikao cha faragha kuhusiana na haliilivyo nchini humo. Balozi wa Uingereza kwenye Umoja huo Barbara Woodward alisema baada ya kikao hicho kwamba Perthes alikuwa mkweli kwenye taathimini yake kwamba dirisha la mazungumzo na suluhu ya amani sasa limefungwa. Hata hivyo amesema baraza hilo bado linasisitiza kuendelezwa kwa mazungumzo.

Soma Zaidi: Juhudi za suluhu Sudan, zaendelea 

Sudan imekabiliwa na ubadilishanaji tete wa mamlaka tangu vuguvugu la wanaounga mkono demokrasia la mwaka 2019 yaliyosababisha kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir na hatimaye kwa mara ya kwanza kuundwa kwa baraza hilo, baada ya jeshi kusaini makubalino ya kushirikishana madaraka na vikundi vinavyounga mkono demokrasia.

Mashirika: APE