Kesi dhidi ya Chauvin yaanza kusikilizwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kesi dhidi ya Chauvin yaanza kusikilizwa

Hatimaye kesi dhidi ya aliyekuwa afisa wa polisi Dereck Chauvin inaanza kusikilizwa hii leo nchini Marekani, ikiwa ni karibu mwaka mmoja sasa tangu kifo cha George Floyd. Chauvin anatuhumiwa kusababisha kifo cha Floyd.

Hatimaye kesi dhidi ya aliyekuwa afisa wa polisi Dereck Chauvin inaanza kusikilizwa hii leo nchini Marekani, ikiwa ni karibu mwaka mmoja sasa tangu kifo cha George Floyd. Chauvin anatuhumiwa kwa kusababisha kifo cha Mmarekani huyo mweusi baada ya kumkandamiza kwa goti kwa muda wa takribani dakika nane. 

Dereck Chauvin,mtuhumiwa mkuu kwenye kesi hiyo anakabiliwa na mashtaka kadhaa ambayo ni pamoja na mauaji ya kukusudia, ambayo hukumu yake ni hadi kifungo cha miaka 40 jela, katika jimbo la Minnesota.

Mchakato wa kesi hiyo inayosikilizwa katika mji mkuu kwenye jimbo hilo, unatarajiwa kuanza kwa kuchagua jopo la majaji na ambao unaweza kuchukua wiki tatu, lakini kesi yenyewe itaanza kusikilizwa rasmi Machi 29.

Kifo cha George Floyd, Mmarekani mweusi ambaye hata hakuwa na silaha kilichochea maandamano makubwa ndani na nje ya Marekani mwaka jana, yaliyolaani matumizi ya nguvu yanayofanywa na polisi dhidi ya raia, lakini pia ubaguzi wa rangi nchini humo.

Weltspiegel 08.03.2021 | USA | Black Lives Matter Protest in Minneapolis

Baadhi ya waandamanaji katika mji wa Minneapolis waliojitokeza siku moja kabla ya kuanza kusikilizwa kesi dhidi ya afisa polisi Dereck Chauvin

Jana Jumapili kulifanyika maandamano katika mitaa ya Minneapolis, yaliyopewa jina "I cant Breath" ama "Nashindwa kupumua" kwa lengo la kushinikiza haki. Mmoja ya waandamanaji, ambaye ni mkazi wa Minneapolis aliyeishi katika eneo hilo kwa takriban miaka sita alizungumza na vyombo vya habari akisema

"Hii ni hatua kubwa kuelekea mapinduzi ya upatikanaji wa haki kwa watu wa mataifa mengine na kwenye mfumo wa kisheria, na hasa hapa Minneapolis." alisema mwandamanaji huyo.

Floyd, alifariki dunia Mei 25 mwaka jana akiwa ni miaka 46 baada ya kukamatwa na polisi kwa madai ya kulipa bili kwa kutumia dola bandia. Maafisa wa polisi walimkandamiza ardhini na Chauvin alimuwekea goti kwenye shingo kwa dakika nane, huku Floyd akiomba angalau aondoe goti lake ili aweze kupumua, hii ikiwa ni kulingana na picha zilizoonyesha tukio la kukamatwa kwake.

Matokeo ya uchunguzi yalionyesha, Floyd alipoteza fahamu na hatimaye kufariki dunia.

George Floyd azikwa Houston

Chauvin, afisa mzungu wa polisi aliyefukuzwa kazi kufuatia tukio hilo na baadae kuachiwa kwa dhamana, pia anakabiliwa na mauaji ya kutokukusudia na ikithibitika atakabiliwa na miaka mingine kumi ya nyongeza jela.

Ulinzi umeimarishwa kwenye eneo la mahakama itakaposikilizwa kesi hiyo kutokana na wasiwasi wa kuibuka maandamano. Wanasheria wa Chauvin wanasisitiza kwamba mteja wao alifuata kikamilifu taratibu alizoelekezwa mafunzoni wakati anapotakiwa kuwasaidia wenzake wanapomkamata mhalifu.

Maafisa wengine watatu wa zamani wa polisi waliohusika na tukio hilo wanakabiliwa na madai ya kusaidia kufanyika mauaji hayo ya kutokukusudia. Mashitaka dhidi yao yanatarajiwa kuanza kusikilizwa Agosti 23.

Mashirika: DPAE/RTRE