Kenyatta na Macron wafungua mkutano wa mazingira Nairobi | Matukio ya Afrika | DW | 14.03.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenyatta na Macron wafungua mkutano wa mazingira Nairobi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye yumo barani Afrika kwa ziara rasmi, siku ya Alhamis amewahutubia wajumbe wa mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira unaofanyika jijini Nairobi.

Macron ambaye amewasili Jumatano nchini Kenya akitokea Ethiopia, pia alikutana na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi, ambapo aliahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi zote mbili na katika vita dhidi ya ugaidi.

Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo wa mazingira unaoendelea katika makao makuu ya mpango wa mazingira wa Shirika la Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Macron amesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kimataifa za kuhifadhi mazingira ili kuepukana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

"Ulimwengu wa sasa umeshikamana. Tumeunga kwa dhati kwa sababu kila mmoja wetu aliyeko hapa ni sehemu ya harakati za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi au kwa njia nyingine dhidi ya uchafuzi wa mazingira. Wakati tulipoamua kuanzisha mchakato huu mnamo Desemba 2017 baadhi ya watu waliamua kujiondoa baada ya mkataba wa Paris", alisema Macron.

Kiongozi huyo amesema taifa lake lipo tayari kusaidia mataifa yanayoendelea hasa barani Afrika kufikia malengo yake ya kuzalisha na kukuza matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Kenia Nairobi - Emmanuel Macron beim One Planet Summit (Getty Images/AFP/L. Marin)

Rais Macron akitia saini tamko baada ya kumalizika mkutano wa mazingira

Rais Macron pia ametuma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa wajumbe waliokufa kwenye ajali ya ndege mwishoni mwa wiki. Wajumbe wapatao 22 kutoka mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa waliangamia wakati ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia ilipoanguka viungani mwa jiji la Addis Ababa na kuwaua abiria wote waliokuwemo pamoja na rubani na wahudumu wake.

Mbali na Macron, wakuu wengine wa nchi wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja na Marais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Andry Rajoelina wa Madagascar na Maithripala Sirisena wa Sri Lanka na mwenyeji wao Rais Kenyatta.

Naye Rais Kenyatta amesema Kenya ipo imara kushirikiana na jumuiya ya ulimwengu katika ijtihada za kutunza na kuhifadhi mazingira.

"Leo tuko hapa kuapa na kuwahakikishia kwa niaba ya serikali na Wakenya wote kwa jumla kwamba tumekata kauli kufikia mwaka wa 2022 tunataraji kuongeza misitu yetu kwa asilimia 10 kama njia mojawapo ya kutekeleza majukumu yetu kama serikali na kama wanachama wa jumuia ya kimataifa".

Mkutano huo, ambao ni kikao cha nne cha programu ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira, unawashirikisha zaidi ya wajumbe 4,700, wakiwepo mawaziri, wanadiplomasia na wanaharakati wa kutetea uhifadhi wa mazingira.