1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kupima COVID 19

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi.29 Aprili 2020

Taifa la Kenya linakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kuchunguza na kupima ugonjwa wa covid-19, huku serikali ikionya kuwa huanda watu 30000 wakafa hali ikiwa mbaya zaidi.

https://p.dw.com/p/3bYPH
Kenia Coronavirus  Uhuru Kenyatta Meeting
Picha: PSCU

Taasisi ya Utafiti wa matibabu inahitaji shilingi milioni 790 ili kununua vifaa hivyo vinavyohitajika kwa dharura.

Kwenye mkutano na kamati ndogo ya bunge la seneti inayoshughulikia ugonjwa wa Covid-19, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafti wa Matibabu Nchini Yeri Kombe amesema kuwa taasisi hiyo imeishiwa na vifaa pamoja na kemikali zinazohitajika kupima na kuwachunguza wagonjwa. Ufichuzi huo unajiri wakati wizara ya Afya ikisema ilikuwa imetenga shilingi bilioni 2.1 kukabiliana na janga hili. Fedha hizo zinajumuisha shilingi bilioni moja kutoka kwa serikali na Benki ya Dunia. Kenya inaiomba Benki ya Dunia kima kingine cha shilingi bilioni tano, huku maswali yakizidi kuulizwa kuhusu matumizi ya fedha hizo.

"Natilia mkazo umuhimu wa kupima. Ni vyema kuwa na huo uwezo, ili kufahamu jinsi ugonjwa huo ulivyosambaa nchini. Lakini nakubali kuwa kuna changamoto ya vifaa.” Amesema Mohammed Kuti ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Afya katika baraza la magavana.

Taasisi hiyo ya Utafiti wa Matibabu imewapima zaidi ya wagonjwa 6000 tangu kulipuka kwa virusi vya Corona mwezi Machi. Changamoto inazozikabili sasa zinatishia kulemaza vita dhidi ya ugonjwa huo ambao unasambaa kwa haraka huku jumla ya watu 374 wakiripotiwa kuugua, huku wengine 124 wakipona kabisa na wengine 14 wakiaga dunia.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na mawaziri wengine akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vita dhidi ya corona. (Picha ya maktaba Machi 15,2020)
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na mawaziri wengine akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vita dhidi ya corona. (Picha ya maktaba Machi 15,2020)Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/D. Sigwe

Akielezea matumizi ya fedha hizo, Kombe ameelezea kuwa taasisi hiyo inahitaji shilingi milioni 100 za kuajiri wataalamu watakaosaidia kuboresha kasi ya utendajikazi. Shilingi milioni 540 za kununua kemikali na vifaa pamoja na kusaidia kwenye utafiti wa chanjo ya ugonjwa huo. Kwa wastani watu 700 hupimwa kwa siku badala ya 37000 kutokana na uhaba wa vifaa.

"Kuhusu upimaji wa watu wengi, zoezi hilo linaendelea, linalenga watu walioko kwenye hatari, wakiwemo maafisa wa matibabu. Kwa sasa tuna vifaa elfu 25 vya kupima, vitakavyotumika.” Amesema Mutahi Kagwe ambaye ni waziri wa Afya.

Kamati ndogo ya seneti inayokabiliana na janga hili, imependekeza kuwa fedha hizo zitolewe kwenye bajeti ndogo ili kuboresha utafiti na kununua vifaa vinavyohitajika. Hayo yanajiri wakati mkurugenzi mkuu wa Utafiti wa Taasisi hiyo Dr Joel Lutomiah akipigwa kalamu.

Kamati hiyo imesema kuwa hatua hiyo huenda ikavunja nia na ari ya wafanyikazi hivyo kuwa na athari kubwa kwa utekelezaji wa majukumu. Daktari huyo alitimuliwa kwa kuchelewesha matokeo ya utafiti.