Kenya yachagua timu yake ya Olimpiki | Michezo | DW | 04.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kenya yachagua timu yake ya Olimpiki

Timu ya Kenya itakayoelekea Rio katika Michezo ya Olimpiki imekita kambi ya mazoezi mjini Eldoret ambako wanamichezo watayanoa makali kabla ya kwenda kusaka medali mwezi ujao

Kikosi hicho dhabiti chenye wanamichezo 50 kitaongozwa kwa mara nyingine na nahodha Ezekiel Kemboi. Kemboi aliingoza TeamKenya katika kutwaa taji la dunia mjini Beijing mwaka jana.

Kenya iliponea chupuchupu kufungiwa nje ya Olimpiki kutokana na kashfa ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu misuli miongoni mwa wanariadha wake. Jackson Tuwei rais wa chama cha riadha cha Kenya anasema ni wanariadha safi pekee watakaoiwakilisha Kenya mjini Rio "Kulikuwa na sintofahamu, na mashaka, na wasiwasi kwa sababu ya tuhuma mpya. Kwa sababu sio kila mwanamichezo nchini Kenya ambaye anadaiwa kutumia dawa zilizopigwa marufuku. Tuna rekodin za waliotuhumiwa kufanya hivyo na wameonywa kwa mujibu wa sheria za WADA, IAAF na hawako kwenye timu ya taifa".

Tuwei ameahidi kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC na Shirika la Kimataifa la Riadha – IAAF kuhakikisha kuwa kuna mfumo imara wa kufanya vipimo vya dawa zilizopigwa marufuku michezoni "Nadhani ni suala la kuushawishi ulimwengu kuwa wanamichezo wa Kenya ni safi. Kama wana wasiwasi wowote, hatuna tatizo, tutashirikiana nao. tutazingatia sheria zote za WADA, IAAF na wakati wowote wakitaka kuwapima wanamichezo wetu, tutawaruhusu kwa sababu hatutaki kuonyesha mashaka yoyote kuhusu usafi wa wanariadha wetu. Tunataka kumwonyesha kila mtu ulimwenguni kuwa wanariadha wetu ni safi na wako tayari kushindana kwa njia safi".

Nchi hiyo ilipitisha sheria kali ya kupambana na wanariadha na maafisa wanaohusika na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga