Kenya: watatu wakamatwa kwa njama za shambulizi la kimeta | Matukio ya Afrika | DW | 04.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya: watatu wakamatwa kwa njama za shambulizi la kimeta

Polisi nchini Kenya imewakamata watu watatu wanaoshukiwa kupanga njama za kutekeleza shambulizi la kigaidi, la kutumia kemikali za kibayolojia zenye bakteria wa maradhi ya kimeta.

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa Kenya, Joseph Boinnet washukiwa hao ambao ni wanaume wawili na mwanamke mmoja waliokamatwa Ijumaa iliyopita, ni wanachama wa tawi la kigaidi kwa Afrika Mashariki lenye mafungamano na kundi la IS.

Hata hivyo shutuma za polisi dhidi ya ukamataji wa washukiwa wanaohusishwa na ugaidi mara nyingi hukabiliwa na upinzani kutoka upande wa mashirika ya haki za binaadamu.

Boinnet ameeleza washukiwa hao wanadaiwa kuhusika katika njama za kufanya mashambulizi ya kiwango kikubwa, kwa kutumia kemikali zenye bakteria wanaosababisha maradhi ya kimeta.

Mohammed Abdi Ali anayedaiwa kuongoza kundi hilo ambaye pia ni mwanafunzi wa masomo ya udaktari kutoka taasisi ya mafunzo ya Wote, kusini-mashariki mwa mji mkuu wa Nairobi, amekamatwa na atawekwa kizuizini kwa muda wa siku 30 huku uchunguzi ukiwa unaendelea kutafuta ushahidi zaidi.

Watu wengine wawili wanaodaiwa kuwa washirika wake -- mke wake Nuseiba Mohammed Haji, amabye pia ni mwanafunzi wa masomo ya matibabu, na mwanamke mwengine Fatuma Mohammed Hanshi -- walikamatwa nchi jirani ya Uganda.

Washukiwa wengine wawili, Ahmed Hish na Farah Farah Dagne, amabo pia ni wanafunzi wa masomo ya kitabibu. Hadi sasa watuhumiwa hao bado wanasakwa, na polisi wamesema watatoa zawadi ya kiasi cha dola za Marekani 20,000 kwa kutoa habari zitakazowezesha kukamatwa kwa washukiwa hao wanaosakwa.

Mashirika ya haki za binaadamu yakosoa

Nairobi Kenia Abgeordnete Parlament Debatte Sicherheitsgesetz 18.12.2014

Afisa wa polisi nchini Kenya

Wakati hayo yakiendelea, shutuma za polisi mara nyingi zimekuwa zikikosolewa na mashirika ya haki za binaadamu.

"Polisi hapa Kenya wana mtindo wa kukamata watu na kuwaweka ndani halafu ndio wakaiomba mahakama ili wapate muda kuwachunguza. Hawashiki watu wakiwa na uthibitisho wa kuhusika na kosa. Na mara nyingi utaona kuwa watu wanapelekwa mahakamani na wanakaa siku nyingi ama miezi mingi na baadae huwachiliwa huru kutokana na ukosefu wa ushahidi," amesema Khelef Khalifa, mkurungenzi wa shirika la Waisilamu la Kutetea Haki za Binaadamu MUHURI.

Boinnet ameongeza kulingana na uchunguzi wa awali wa polisi, Ali anatuhumiwa kuwashawishi vijana wa vyuo vikuu vya Kenya kujiunga na makundi ya kigaidi.

Aidha duru za ujasusi wa nchi za nje zimethibitisha kwamba Ali anahusika na kundi la kigaidi la IS, lakini zaidi anahusika katika kukusanya wapiganaji wanaotumwa katika nchi za Libya na Syria na sio kwa lengo la kufanya mashambulizi nchini Kenya.

Polisi nchini Kenya wamelifananaisha shambulizi hilo lilopangwa kufanywa na lile la Septemba 2013, katika jengio la biashara la Westgate la mjini Nairobi Kenya lilohusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda lilosababisha vifo vbya zaidi ya watu 67.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe

Mhariri: Yusuf Saumu