1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu mkuu wa UN: Demokrasia ya dunia imetekwa nyara

Saumu Mwasimba
25 Septemba 2018

Antonio Guterres ameuonya ulimwengu juu ya kuoneshana ubabe na kutekwa nyara kwa demokrasia wakati ambapo walimwengu wakiwa wamepoteza imani na taasisi zao huku makundi ya kizalendo yakiongezeka.

https://p.dw.com/p/35TrD
Antonio Guterres
Picha: picture-alliance/AP Images/R. Drew

Kikao cha  hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kimefunguliwa rasmi kwa hotuba ya katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres mjini Newyork.Miongoni mwa mambo aliyoyagusia katika hotuba yake amesema misingi ya demokrasia duniani  imetekwa nyara.

Ulimwengu unakabiliwa na hali mbaya ya kukosekana hali ya kuaminiana wakati demokrasia ikihujumiwa.Hivyo ndivyo anavyouangalia ulimwengu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye hivi punde ameunfungua rasmi mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa na kuhutubia viongozi mbali mbali kutoka nchi 133 za dunia wanaohudhuria mjini NewYork. Kupitia hotuba yake ameutolea mwito ulimwengu kurudisha imani katika suala zima la kuaminiana katika wakati huu ambapo ulimwengu unakabiliwa na matatizo chungunzima kuanzia mabadiliko ya tabia nchi hadi ugaidi na migogoro. Guterres amewaonya viongozi kwamba kanuni za ulimwengu zinazidi kuvurugika wakati imani ikiwa katika kilele cha kuporomoka huku mabadiliko katika wizani wa madaraka ukitishia kuongeza kitisho cha kuzuka vita.

''Dunia yetu inakabiliwa na hali mbali ya ukosefu wa hali ya kuaminiana,watu wanamashaka na hofu.Na hali ya uaminifu imefikia ukingoni.Iwe ni uamunifu kwenye taasisi za kitaifa,uaminifu miongoni mwa mataifa na uaminifu katika sheria za kimataifa.Ndani ya nchi watu wanapoteza imani na mifumo ya kisiasa.Uimla umeongezeka na makundi ya siasa kali za kizalendo nayo yanaibuka.''

Hata hivyo mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa hakumlaumu yoyote moja kwa moja kwenye hutuba yake hiyo lakini mkutano huu wa viongozi wa dunia unafanyika katika wakati ambapo pia hali ya mvutano inazidi kutokota  kati ya Marekani na Iran.Rais Donald Trump anajiandaa muda wowote kutoka sasa kuutangazia ulimwengu kupitia jukwaa hilo la hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa jinsi anavyoulinda uhuru wa nchi yake.

UN Versammlung Antonio Guterres
Picha: Getty Images/AFP/T. A. Clary

Lakini katika hotuba yake katibu mkuu Guterres amewaonya viongozi wa dunia kutoeneza siasa za vitisho akisema kwamba wale wanaodhani kwamba majirani zao ni  hatari huenda wakasababisha kitisho pale ambapo hapakuwa nacho. Hilo ameligusia kuonesha pia wasiwasi uliopo kuhusu suala la wakimbizi ambapo ameweka wazi kwamba wale wanaofunga mipaka yao kuzuia wakimbizi kuingia kwenye nchi zao  mara kwa mara wanachokifanya sio kitu kingine bali tu ni kuchochea ongezeko la watu wanaofanya biashara haramu ya usafirishaji watu kwa njia za magendo.

Lakini pia amewageukia wale wanaopuuza haki za binadamu katika suala zima la kukabiliana na ugaidi akisema kwamba kutozingatia haki za binadamu kwenye mapambano hayo ni hatua inayochangia kuota kwa kasi kwa makundi ya itikadi kali. Ulimwengu unahitaji mshikamano wa viongozi katika kuimarisha amani,haki za binadamu na maendeleo endelevu huo ndio mwito aliousisitiza katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/rtre/afp

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman