Karzai aimbia Loya Jirga haiamini Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Karzai aimbia Loya Jirga haiamini Marekani

Rais Hamid Karzai amefungua baraza la Loya Jirga, akiwataka wazee wa kibabila kuunga mkono mkataba wa usalama kati ya nchi yao na Marekani, huku wakijua kwamba imani baina ya pande hizo mbili ni ndogo sana.

Rais Hamid Kazrai wa Afghanistan akifungua mkutano wa Loya Jirga siku ya tarehe 21 Novemba 2013.

Rais Hamid Kazrai wa Afghanistan akifungua mkutano wa Loya Jirga siku ya tarehe 21 Novemba 2013.

Baraza hili linalowajumuisha wajumbe 2,500, linakutana siku moja tu baada ya Karzai na serikali ya Marekani kufikia makubaliano juu ya mkataba unaoelezea hadhi ya wanajeshi wa Marekani watakaokuwepo baada ya kujiondoa rasmi kwa kikosi cha Jumuiya ya Kujihami ya NATO hapo mwaka 2014.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa jana (20 Novemba), wanajeshi wa Marekani watakaofanya uhalifu nchini Afghanistan baada ya mwaka 2014, watapewa kinga kutoka sheria ya Afghanistan, ikimaanisha kwamba wanajeshi hao watashitakiwa tu kwa mujibu wa sheria za Marekani na sio za Afghanistan.

Hiki kilikuwa ni kizingiti kikubwa kilichotanza kufikiwa kwa makubaliano hayo kwa takribani mwaka mzima. Tayari viongozi wa kikabila na kisiasa, waliosafiri kutoka pande zote za nchi kuhudhuria mkutano huo, wameelezea hasira zao juu ya namna makubaliano hayo yalivyofikiwa.

Karzai hana imani na Marekani

Wajumbe wa baraza la Loya Jirga katika kikao kilichoanza tarehe 21 Novemba 2013 mjini Kabul, Afghanistan.

Wajumbe wa baraza la Loya Jirga katika kikao kilichoanza tarehe 21 Novemba 2013 mjini Kabul, Afghanistan.

Karzai mwenyewe aliwaambia wajumbe hao, ambao sasa wanayajadili makubaliano hayo kwamba hana imani na Marekani. "Imani yangu kwa Marekani si nzuri. Siwaamini, hawaniamini. Kwa miaka 10 iliyopita, nimepigana pamoja nao na wao wamesambaza propaganda dhidi yangu," alisema.

Pamoja na kujadili makubaliano hayo, baraza hilo la wazee linajadili pia ikiwa wanajeshi wa Marekani wataendelea kubakia au kuviwacha vikosi vya Kiafghani kupambana na waasi wa Taliban baada ya mwaka ujao. Hilo likikubalika, mjadala utasalia kwenye idadi ya wanajeshi na vituo vya kijeshi vya Marekani.

Nakala ya makubaliano hayo yanayojuilikana kwa kifupi kama BSA imesambazwa kwa wajumbe wote wa kikao hiki cha siku nne, kwa mujibu wa waandaaji.

Marekani yasema makubaliano yameafikiwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.

Masaa kadhaa kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alisema mjini Washington kwamba pande hizo mbili zilikubaliana juu yaliyoandikwa kwenye makubaliano hayo kupitia mazungumzo ya simu na Karzai.

Serikali ya Afghanistan imetangaza mapumziko ya siku sita, yaliyoanzia juzi Jumanne, kwa ajili ya maandalizi ya mkutao huu wa Loya Jirga.

Eneo ambalo mkutano huo unafanyika liko chini ya ulinzi mkali. Maelfu ya maafisa wa usalama wamesambazwa mji mzima, huku kukiwekwa vizuizi vya barabarani katika njia zote zinaoingia mjini Kabul.

Taliban inalikosoa baraza la Loya Jirga na kuliita la kipuuzi. Mwaka 2011, walirusha maroketi mawili kwenye hema ambako lilikuwa likifanyika lakini wakawakosa wajumbe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com