1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson kushinikiza tena uchaguzi Uingereza

Yusra Buwayhid
29 Oktoba 2019

Waziri Mkuu wa Uingereza anatarajiwa Jumanne kujaribu tena kulazimisha uchaguzi wa mapema, licha ya wabunge kuukataa mpango wake, kufuatia Umoja wa Ulaya kukubali kuiongezea mchakato wa Brexit muda wa miezi mitatu.

https://p.dw.com/p/3S7KO
Großbritannien London Parlament Brexit
Picha: picture-alliance/empics/House of Commons

Wabunge jana kwa mara ya tatu wamelikataa pendekezo la Boris Johnson la kuitisha uchaguzi wa mapema. Johnson pia alipata pigo kubwa mapema jana pale alipolazimika kukubali mchakato wa Brexit kucheleweshwa badala ya kutekelezwa Oktoba 31 kama ilivyopangwa awali. Aliwahi kusema anahiari kufariki kuliko kurefusha mchakato wa Brexit ulioanzishwa mwaka 2016 kufuatia kura ya maoni.

Matumaini ya serikali ni kwamba uchaguzi unaweza kumaliza mkwamo wa kisiasa, lakini chama kikuu cha upinzani, Labour, kinachopinga mpango wa Brexit wa Johnson, kimesema hakitounga mkono kufanyika uchaguzi hadi pale kitisho cha waziri mkuu huyo cha kuiondoa Uingrezea katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano yoyote kitakapofutwa kabisa. Kiongozi wa chama hicho Jeremy Corbyn ameliambia bunge kwamba waziri mkuu wao ni mtu asiyeaminika, ambaye kila ahadi aliyoitoa hakuweza kuitimiza.

"Anakwepa majukumu yake. Anavunja ahadi zake kujiepusha kuchunguzwa. Na leo anataka kuidhinishwe uchaguzi pamoja na mpango wake. Hatopata idhini yetu. Anasema anataka uchaguzi tarehe 12 Desemba. Je! Tunawezaje kumwamini,?" aliuliza Corbyn.

Großbritannien London Parlament Brexit Jeremy Corbyn
Kiongozi wa chama cha upinzani Labour, Jeremy CorbynPicha: picture-alliance/empics/House of Commons

Serikali kujaribu tena

Johnson jana alikikosoa vikali chama cha upinzani cha Labour baada ya kuashiria nia yake ya kupinga kura dhidi ya uchaguzi mkuu wa Desemba 12.

Soma zaidi: Brexit hadi Januari 31, 2020

Pendekezo hilo lilishindwa kupitishwa bungeni baada ya kukosa kura 434 zilizohitajika, ambazo ni sawa na theluthi mbili ya kura zote bungeni. Badala yake limeungwa mkono kwa kura 299 na kupingwa kwa kura 70.

Johnson alimlenga kiongozi wa Labour Jeremy Corbyn kwa kukataa kuunga mkono kuitishwa uchaguzi mkuu, akisema kuwa anaweza kukimbia lakini hawezi kujificha. Kwani bungeni anaowadhania washirika wake wameanza kumtenga.

Vyama vidogo vya upinzani, kama vile Liberal Democrats na Scottish National Party (SNP), vimeonyesha nia ya kuunga mkono uchaguzi mkuu, ingawa sio kupitia pendekezo la serikali.

Serikali hata hivyo inakusudia kujaribu tena kupendekeza uchaguzi kupitia kura nyingine inayohitaji wingi mdogo wa kura bungeni, ikiwezekana mapema leo. Katika barua yake kwa Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk, Johnson alizihimiza nchi wanachama wa umoja huo kuweka wazi kwa wabunge kwamba muda hauwezi tena kurefushwa baada ya siku ya mwisho ya Januari 31, ikiwa bunge la Uingereza litapinga pendekezo lake la kuitisha uchaguzi mkuu.

afp, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Pakistan Anschlag in Quetta
Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW
Nenda ukurasa wa mwanzo