Jeshi la Nigeria lawaokoa watu 178 kutoka kwa Boko Haram | Matukio ya Afrika | DW | 03.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jeshi la Nigeria lawaokoa watu 178 kutoka kwa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limewaokoa watu 178 wakiwemo watoto mia moja ambao walikuwa wameshikwa mateka na waasi wa kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Msemaji wa jeshi la Nigeria, Kanali Tukur Gusau, amesema wanajeshi wamewaokoa watu 178 kwa jumla, watoto 101, wanawake 67 na wanaume kumi kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Boko Haram wakati wa operesheni kali dhidi ya waasi hao.

Operesheni hiyo, ambayo jeshi limesema pia lilimkamata mmoja wa makanda wa Boko Haram, ilifanyika karibu na eneo la Bama yapata kilomita sabini kusini mwa mji wa Maiduguri kaskazini mwa Nigeria.

Jeshi lafanya operesheni kali

Kambi kadhaa za Boko Haram pia ziligundulika na kuharibiwa na wanajeshi katika mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri, ambao ni kitovu cha uasi huo unaofanywa na Boko Haram.

Wanejeshi wa Nigeria wakishika doria kaskazini mwa Nigeria

Wanejeshi wa Nigeria wakishika doria kaskazini mwa Nigeria

Jeshi hilo la Nigeria pia limesema hapo jana lilifanya mashambulizi ya angani kaskazini mashariki mwa nchi hiyo katika kijiji cha Bita kuwasambaratisha waasi hao wa Boko Haram ambao idadi kubwa kati yao inasemekana wameuawa katika shambulizi hilo.

Boko Haram hapo jana nayo ilitoa vidio mpya katika mtandao wa Twitter inayoonyesha ilifanya mashambulizi katika majimbo ya Borno na Yobe yaliyozilenga kambi za kijeshi na pia vidio hiyo ilionyesha kuuawa kwa mwanamume aliyekuwa amevaa magwanda ya sare za jeshi anayesemekana kuwa mwanajeshi wa Nigeria.

Mkulima mmoja wa eneo hilo Moha Saleh amesema watu 13 wameuwa na wengine 27 wamejeruhiwa katika hsmabulizi hilo la Jumapili ambalo lilianza wakati waasi hao walipokivamia kijiji hicho kuchoma nyumba kadhaa kwa tuhuma kuwa wakaazi wa kijiji hicho wametoa taarifa kwa wanajeshi kuhusu waliko waasi.

Boko Haram yadai kuwashambulia wanajeshi

Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Nigeria limewaokoa mamia ya watu ambao wamekuwa mateka wa waasi wa Boko Haram hasa waliokuwa wakizuiwa katika msitu mkubwa wa Sambisa ambao ni mojawapo ya ngome kuu ya kundi hilo lenye mafungamano na wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS. Wiki iliyopita watu 71 waliokolewa pia na wanajeshi.

Wanamgambo wa Boko Haram

Wanamgambo wa Boko Haram

Tangu mwaka 2009, zaidi ya watu 15,000 wameuawa kufuatia uasi ulioanzishwa na waasi hao wa Boko Haram na kundi hilo katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni limetanua uasi wake hadi nchi jirani na Nigeria zikiwemo Cameroon, Niger na Chad.

Nigeria na nchi hizo jirani zinapanga kuanzisha kikosi cha pamoja cha kijeshi kupambana dhidi ya waasi hao katika kanda hiyo. Kikosi hicho kitakuwa na wanajeshi 8,700 na kinatarajiwa kuanza kuhudumu hivi karibuni.

Rais wa Niger Mahamadou Issoufou ameeleezea matumaini kuwa kikosi hicho kipya kitafanikiwa katika kulitokomeza kundi hilo ambalo limezorotesha usalama katika kanda hiyo.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/dpa/ap

Mhariri: Mohammed Khelef