Jeshi la Misri lakabiliana na wapiganaji Sinai | Matukio ya Afrika | DW | 09.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jeshi la Misri lakabiliana na wapiganaji Sinai

Jeshi la Misri limesema ndege zake zimeshambulia maficho na maghala ya silaha ya makundi ya kigaidi na uhalifu, muda mfupi baada ya serikali kutanga opereshini kubwa dhidi ya ugaidi katika rasi ya Sinai.

Kanali Tamer al-Rifai alisema katika taarifa kupitia televisheni kwamba operesheni hiyo itafanyika katika maeneo mengi ya Rasi ya Sinai, na pia baadhi ya maeneo ya mkoa wa Nile Delta na jangwa la magharibi.

Vikosi vya usalama vya Misri vimepambana na waasi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu kwa miaka kadhaa katika mkoa wa Sinai Kaskazini, ambao wamewaua mamia ya wanajeshi na polisi.

Wapiganaji hao wamepanua shabaha zao na kuwajumlisha raia katika mwaka uliopita. Operesheni hiyo inakuja wiki kadhaa kabla ya uchaguzi wa rais wa Machi 26 hadi 28, ambamo rais Abdel-Fattah al-Sissi anawania mhula wa pili.

Karte Infografik Ägypten mit Nord Sinai

Ramani ya Misri ikionyesha rasi ya Sinai ambako jeshi limeanzisha operesheni dhidi ya ugaidi na uhalifu.

"Kwa maagizo ya rais na amiri jeshi mkuu wa majeshi, asubuhi ya leo vikosi vya usimamizi wa sheria vimeanzisha mpango wa kukabiliana na makundi ya kigaidi na uhalifu kaskazini na katikati mwa Sinai, maeneo mengine ya karibu na Delta ya Misri na kipande cha jangwa magharibi mwa Mto Nile, kwa lengo kuimarisha udhibiti wa njia za kutokea taifa la Misri, na kuyasafisha maeneo hayo na maficho ya magaidi, na kuwalinda watu wa Misri dhidi ya maovu ya ugaidi na itikadi kali," alisema Kanali Al-Rifai.

Usalama waimarishwa mipakani

Chanzo cha usalama katika mkoa wa Sinai Kaskazini kimesema vikosi vya polisi na jeshi vilikuwa vinaisafisha rasi hiyo, baada ya kufunga njia zote za kutokea ili kuzuwia mshukiwa yeyote kutoroka. Chanzo hicho kimeilezea operesheni hiyo kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa na jeshi katika rasi hiyo mpaka sasa. Mashuhuda waliliambia shirika la habari la Ujerumani DPA, kwamba miripuko ilisikika katika maeneo kadhaa ya Sinai.

Askari wa ulinzi wa mipaka na vikosi vya polisi wameripotiwa kuimarisha hatua za usalama kwenye mipaka, huku vikosi vya jeshi vikiimarisha uwepo wake katika kile ambacho jeshi limekieleza kuwa maeneo muhimu ya nchi. Vikosi vya majini pia vimeimarisha usalama katika mipaka ya baharini, ili kuwakatia ugavi magaidi, limesema jeshi hilo.

Ägypten Präsident Abdel Fattah Al-Sisi (picture-alliance/dpa/K. Elfiqi)

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi.

Ongezeko la mashambulizi ya wapiganaji

Misri imepambana na uasi katika rasi ya Sinai tangu mapinduzi ya umma ya mwaka 2011, yaliomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Hosni Mubarak. Lakini mashambulizi ya wapiganaji - yakilenga hasa vikosi vya usalama na jamii ya wakristo wachache nchini humo, yaliongezeka baada ya jeshi kumpindua rais wa kwanza aliechaguliwa kidemokrasia Mohammed Mursi mwaka 2013.

Mengi ya mashambulizi hayo, yaliyofanyika katika sehemu ya kaskazini ya Rasi ya Sinai kwenye mpaka na Israel na Ukanda wa Gaza, yamedaiwa kufanywa na wapiganaji wenye mafungano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, rtrtv

Mhariri: Grace Patricia Kabogo