1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Libya latangaza kudhibiti Tripoli

John Juma
4 Juni 2020

Vikosi vya serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa vimesema vimedhibiti mji mkuu na mipaka yake yote ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege kutoka kwa wapinzani wanaoongozwa na kamanda Haftar.

https://p.dw.com/p/3dGpl
Wanajeshi wakiwa uwanja wa ndege Tripoli
Picha: picture-alliance/H. Turkia

Mapema leo, msemaji wa jeshi la serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya GNA, Mohammed Gnounou alisema vikosi vya serikali vimechukua udhibiti kamili wa mipaka ya mji wa Tripoli baada ya kuvifurusha vikosi vya Haftar. Aidha jeshi la serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa, limesema kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa Twitter kuwa limechukua udhibiti wa uwanja wa ndege ulioko kusini mwa viunga vya mji wa Tripoli, ambao ulichukuliwa na wapiganaji watiifu kwa Khalifa Haftar. Hadi sasa vikosi vya Haftar havijatoa kauli au tamko lolote kuhusiana na hayo.

Taarifa zaidi:  Libya: Pande hasimu kuanza tena mazungumzo

Mashambulizi ya kudhibiti Tripoli

Vikosi hivyo vya Haftar vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) ambavyo vimekita kambi mashariki mwa nchi hiyo, viliushambulia uwanja huo mwezi Juni mwaka 2019 na kuchukua udhibiti wake, ikiwa ni sehemu ya mashambulizi yake dhidi ya serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli. Pande zote mbili kwenye mzozo huo zilipigana karibu na Tripoli, japo Umoja wa Mataifa ulitangaza mnamo Jumatatu kwamba pande husika kwenye mashamblizi hayo zilikubaliana kuanza tena mazungumzo ya kusitisha vita.

Jenerali Khalifa Haftar
Jenerali Khalifa Haftar Picha: Getty Images/S. Gallup

Mnamo Aprili mwaka uliopita, Haftar aliviamuru vikosi vyake kuchukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli kutoka mikononi mwa serikali ya baraza la kitaifa. Lakini katika wiki za hivi karibuni, oparesheni ya vikosi vyake imepata mapigo.

Mapigano kati ya pande zote mbili yamekuwa yakishuhudiwa, licha ya miito ya kimataifa ya kutaka usitishaji vita na juhudi zaidi zilenge mripuko wa virusi vya corona.

Libya, taifa lenye utajiri wa mafuta, limekuwa katika mgogoro tangu mwaka 2011 wakati aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo, Moamer Gaddafi alipouwawa na utawala wake kupinduliwa. Hadi leo, nchi hiyo imesalia kuwa uwanja wa mapigano kati ya pande zinazohasimiana pamoja na washirika wao kutoka nchi za nje, ikiwemo Urusi na Uturuki.

Fayez al-Serraj kukutana na Rais Tayyip Erdogan

Waziri Mkuu wa serikali ya baraza la kitaifa, Fayez al-Serraj, anatarajiwa kukutana na rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan leo Alhamisi mjini Ankara, ambapo afisa mmoja mkuu wa Uturuki amesema hatua ya kutwaa udhibiti wa Tripoli ni muhimu kabla ya uwezekano wa kuanzishwa mazungumzo ya amani. Afisa huyo ameongeza kuwa Erdogan pamoja na Serraj watazungumzia pia mikakati pamoja na hali ilivyo.

Umoja wa Mataifa ndio una wajibu wa kusimamia mazungumzo ya amani. Lakini mjumbe wake kwa ajhili ya ya Libya Ghassan Salame alijiuzulu mwezi Machi na Baraza la Usalama  la umoja huo bado halijakubaliana kuhusu nani atakayelijaza pengo hilo.

Vyanzo: DPAE, RTRE

Mwandishi: John Juma

Mhariri: Josephat Charo