1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi kuongoza Mali kwa muda

19 Agosti 2020

Nchini Mali wanajeshi walioongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa taifa hilo Ibrahim Boubacar Keita aliyejiuzulu mapema hii leo wametangaza kwamba wataiongoza serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi mpya.

https://p.dw.com/p/3hBO1
Unruhen in Mali | Putschistenführer Ismael Wague
Picha: picture-alliance/dpa/AP/Ortm TV

Wanajeshi hao walianzisha uasi mapema jana katika mji wa Kati, na baadae kuelekea mji mkuu Bamako, umbali wa kilomita 15. 

Kanali-meja Ismael Wague ambaye hadi sasa ni mkuu wa utumishi wa jeshi la Mali ametangaza kupitia kituo cha televisheni cha taifa kuundwa kwa kamati ya kitaifa ya uokozi wa wananchi, CNSP, itakayoongoza taifa hilo la Afrika Magharibi linalokabiliwa na hali tete hadi pale tarehe mpya ya uchaguzi itakapopangwa.

Amesema, mapinduzi ya kijeshi yalikuwa ni ya lazima kwa kuwa serikali ya Keita iliitumbukiza Mali kwenye machafuko na kukosekana kwa usalama. Tamko hilo limekuja masaa machache baada ya Keita kutangaza kujiuzulu katika hotuba ya moja kwa moja iliyorushwa kupitia televisheni, baada ya mapinduzi hayo yaliyoshuhudia wanajeshi wakiwakamata Keita na waziri mkuu wake Boubou Cisse.

Wague alisema "Mvutano wa kijamii na kisiasa umedidimiza utendaji sahihi wa nchi kwa muda mrefu. Maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika tangu uchaguzi uliopita yanathibitisha kuwa nchi haiko sawa. Mali ni nchi kubwa, tajiri na tamaduni zake tofauti, tajiri kwa ardhi yake, utajiri wa watu wake, tajiri wa wanyama na mimea, lakini ambaye uwepo wake kama nchi na taifa unatishiwa katika misingi yake yote ya uasisi."

Ufaransa yaipokea kwa tahadhari taarifa hiyo ya kujiuzulu Keita.

Taarifa ya kujiuzulu Keita ilipokelewa kwa shangwe na waandamaji wanaoipinga serikali katika mji mkuu, Bamako lakini ikipokelewa kwa tahadhari na Ufaransa ambayo Mali iliwahi kuwa koloni lake pamoja na washirika wengine na mataifa ya kigeni.

Mali I Ibrahim Boubacar Keita
Aliyekuwa rais wa Mali Boubacar Keita, akiwa Berlin mwaka 2015.Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana baadae leo kujadili hali inavyoendelea nchini Mali ambako Umoja wa Mataifa una wanajeshi 15,600 wanaolinda amani.

Keita aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka 2013 kwa ushindi wa kishindo na kuchaguliwa tena miaka mitano baadae, bado alikuwa na miaka mitatu ya kuhitimisha awamu yake. Hata hivyo, umaarufu wake umeshuka, na waandamanaji walianza kuingia mitaani wakimshinikiza kuondolewa kwake mwezi Juni.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS iliwahi kupeleka wasuluhishi kujaribisha makubaliano ya serikali ya kitaifa, ingawa mazungumzo hayo yalishindikana, baada ya kudhihirika kwamba waandamanaji wasingekubali chochote zaidi ya Keita kujiuzulu.

Kwenye tangazo lake la kujiuzulu, Keita alisema hangependelea kuona damu inamwagika na hivyo ameamua kuachia ngazi. Aidha, alitangaza kuivunja serikali yake na bunge la kitaifa.

Anguko la kisiasa la Keita, linashabihiana kwa karibu na lile la mtangulizi wake. Amadou Toumani Toure aliondolewa kwa nguvu kwenye wadhifa huo mwaka 2012. Kipindi hicho, mashambulizi yalifanywa na waasi waliokuwa wanataka kujitenga wa kabila ya Tuareg.

Mashirika: APE/DPAE