1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan yaadhimisha miaka 10 ya janga la tsunami

Tatu Karema
11 Machi 2021

Japan leo inaadhimisha miaka 10 tangu kutokea kwa janga baya zaidi la asili katika historia ya nchi hiyo ambalo ni  tetemeko kubwa la ardhi, tsunami na kuyeyuka kwa nyuklia lililoathiri taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3qSll
Japan | Tōhoku-Erd-/Seebeben 2011
Picha: Asashi Shimbun/epa/dpa/picture alliance

Maadhimisho ya muongo mmoja wa janga hilo baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo yatafanywa kupitia hafla nyingi za umma na faragaha huku kimya kikitarajiwa kuadhimishwa mwendo wa saa 14.46 nchini humo hii ikiwa ni saa kamili lilipotokea tetemeko kubwa la ardhi la ukumbwa wa 9.0 katika kipimo cha ritcher mnamo Machi 11 mwaka 2011.

Mjini Tokyo, hafla ndogo itakayozingatia sheria za kuthibiti kuenea kwa virusi vya corona itaandaliwa katika ukumbi wa michezo wakitaifa huku hotuba zikitolewa na mfalme Naruhito na waziri mkuu Yoshihide Suga huku idadi ya wageni waalikwa ikiwa ndogo kuliko kawaida.

Katika matamshi ya kuadhimisha miaka kumi ya janga hilo hapo jana, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupunguza athari za majanga UNDRR Mami Mizutori, aliwaambia wanahabari mjini Geneva nchini Uswisi kwamba janga hilo lilitoa mafunzo makali kuhusu jinsi ya kusimamia athari za majanga . Mizutori ameongeza kusema kuwa  Kadhia nzima ya kuzuia na kujiandaa haijawahi kuwa muhimu zaidi kama sasa dunia inapoishi na ugonjwa wa COVID-19 ambao ni janga lililoandikwa katika mfumo wa kupunguza athari za maafa na maafa yanayohusiana na hatari za kibaolojia.

Japan | Tōhoku-Erd-/Seebeben 2011
Tsunami yakumba eneo la makazi katika mji wa Miyagi, Kaskazini Mashariki mwa JapanPicha: dpa-mag/picture alliance

Siku ya Jumatano na Alhamisi, shughuli ya kuwatafuta waliopotea katika maeneo ya Miyagi na Fukushima zilikuwa zinaendelea huku jamaa za watu hao wakikataa kukata matumaini ya kupata mabaki yao muongo mmoja baadaye. Huenda nafasi ya kufanikiwa ikaonekana kuwa ndogo, lakini wiki iliyopita, mabaki ya mwanamke mmoja aliyepotea tangu mkasa huo wa Tsunami yalitambuliwa katika kile mwanawe wa kiume amekitaja kuwa fursa ya kukabiliana na hisia zake na kuendelea na maisha.

Kiasi cha watu 18,500 waliuawa ama kutojulikana walipo katika janga hilo huku wengi wakisombwa na mawimbi makali yaliofunika maeneo ya Pwani ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo pamoja na tetemeko kubwa zaidi ya ardhi kuwahi kurekodiwa. Kuyeyuka kwa nyuklia katika kiwanda cha nyuklia cha Fukushima Daiichi kulighubika maeneo ya karibu na mionzi, na kuifanya baadhi ya miji kutoweza kukaliwa kwa miaka kadhaa huku maelfu yawatu wakipoteza makazi.