1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yamuua kiongozi mwingine wa Iran

18 Machi 2026

Waziri wa Ujasusi wa Iran Esmail Khatib auwawa na Israel katika mashambulizi yaliyofanywa usiku wa kuamkia Jumatano

https://p.dw.com/p/5AdEF
Waziri wa Ujasusi wa Iran aliyeuliwa na mashambulizi ya Israel
Waziri wa Ujasusi wa Iran aliyeuliwa na mashambulizi ya IsraelPicha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Israel imetangaza kumuua   waziri anayesimamia masuala ya ujasusi Iran, Esmail Khatib , wakati Tehran ikifanya maziko ya pamoja ya maafisa wake waliouliwa, jana Ali Larijani aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa, kamanda wa kikosi cha Basij Gholamreza Soleimani pamoja na mabaharia waliouliwa baada ya kuzamishwa meli ya kivita ya Iran.

Kuuliwa kwa Esmail  Khatib ni pigo jingine kwa Jamhuri hiyo ya kiislamu katika vita hii iliyoanza zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Mashambulio yaliyomuuwa waziri huyo yalifanywa saa chache baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuthibitisha juu ya kuuwawa kwa maafisa  wake wa ngazi za  juu wa usalama Ali Larijani na jenerali Gholam Reza Soleimani.

Mashambulizi ya Israel yamesababisha pia uharibifu na mauaji ndani ya Lebanon
Mashambulizi ya Israel yamesababisha pia uharibifu na mauaji ndani ya LebanonPicha: Ibrahim Amro/AFP/Getty Images

Hivi leo Umma wa Wairan ulikusanyika katika uwanja wa Enghelab mjini Tehran kwa maziko ya viongozi hao wakiwa wamebeba picha za viongozi wao wa juu kuanzia muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ruhollah Musavi Khomeini,  Ayatollah Ali Khamenei mpaka  Mojtaba Khamenei na kupeperusha bendera huku  wakijipiga vifua kama heshima kwa waliouwawa na mashambulizi ya Israel.

Ali Larijani alitazamwa kwa kiasi kikubwa nchini Iran kama mmoja wa watu wenye usemi na aliyekuwa mtu wa karibu zaidi na kiongozi wa Juu aliyetangulia kuuwawa kwenye vita hii, Ayatollah Ali Khamenei na mwanawe Mojtaba Khamenei aliyerithi uongozi.

Urusi yalaani mauaji ya viongozi wa Iran

Urusi  imeonesha kuchukizwa na mauaji ya Larijani, msemaji wa rais Vladmir Putin Dmitry Peskov amesema nchi hiyo inalaani mashambulio ya kuwalenga viongozi wa Iran.

"Hapana shaka yoyote, tunalaani vitendo vinavyolenga kuwadhuru kimwili viongozi hao na tunalaani zaidi kuwauwa na kuwamaliza wawakilishi kwenye utawala wa Jamhuri huru ya Iran na hata wale wa mataifa mengine. Tunalaani kabisa vitendo vya namna hiyo'

 Ali Larijani alikuwa mmoja wa viongozi aliyekuwa na ukaribu mkubwa na Ayatollah Ali Khamenei aliyeuliwa mwanzoni mwa mashambulizi ya Israel na Marekani mjini Tehran
Ali Larijani alikuwa mmoja wa viongozi aliyekuwa na ukaribu mkubwa na Ayatollah Ali Khamenei aliyeuliwa mwanzoni mwa mashambulizi ya Israel na Marekani mjini TehranPicha: Bilal Hussein/AP Photo/dpa/picture alliance

Pamoja na Israel kuendelea na mashambulizi yake ya kuwalenga viongozi ndani ya Iran, Tehran nayo imekuwa ikiendelea kuonesha haijasalimu amri.

Iran yathibitisha kifo cha mkuu wa usalama Larijani katika shambulizi ya Israel

Hivi leo(Jumatano) imefyetuwa makombora kuelekea Israel,mwandishi habari wa AFP amesimulia, kusikia miripuko katika mji wa Tel Aviv, wakati katika  mataifa ya Ghuba, miripuko ikisikika Umoja wa Falme za kiarabu na Qatar na Saudi Arabia ikiripoti kuzuia makombora hayo. Wizara ya mambo ya nje ya Qatar kwa upande mwingine imeilaumu Israel kwa kushambulia visima vyake vya gesi vilivyoko kwenye ghuba ya Uajemi inavyotumia pamoja na Iran.

UAE imelengwa mara kadhaa na mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa Marekani ya Iran
UAE imelengwa mara kadhaa na mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa Marekani ya IranPicha: Fadel Senna/AFP/Getty Images

Mashambulizi ya Israel yameendelea pia kutikisa mji mkuu wa Lebanon Beirut, ripoti zikionesha kwamba jengo moja la makaazi liliharibiwa kabisa katika mji wa Bachoura na majengo mengine mawili pia yalilengwa hukohuko Beirut mapema leo asubuhi ambako takriban watu sita waliuwawa.

Wakati huohuo rais Donald Trump amesema Marekani huenda ikaliacha suala la Usalama wa mlango bahari wa Hormuz, kwa mataifa yaliyokataa wito wake wa kutuma meli za kivita kama Uingereza.