1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaishambulia Lebanon na kuwauwa watu 10

21 Februari 2026

Takriban watu 10 wameuawa na wengine 50 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel kwenye Bonde la Bekaa nchini Lebanon.

https://p.dw.com/p/59BzC
Lebanon Qannarit 2026 | shambulizi
Shambulizi la Israel katika kijiji cha Qannarit nchini Lebanon mnamo Februari 16, 2026Picha: Joseph Eid/AFP

Haya ni kulingana na vyanzo viwili vya usalama vilivyoliarifu shirika la habari la reuters, baada ya jeshi la Israeli kusema kuwa lilikuwa limelenga maeneo ya Hezbollah katika eneo la Baalbek.

Vyanzo hivyo pia vimesema afisa mmoja mkuu wa Hezbollah ni miongoni mwa waliouawa.

Hata hivyo hakukuwa na tamko la haraka kutoka kwa Hezbollah.

Lakini katika taarifa tofauti leo, jeshi hilo la Israel limesema limewauwa wanamgambo kadhaa wa Hezbollah katika kamandi tatu tofauti ambazo ziligunduliwa hivi karibuni kufanya kazi kuharakisha utayari na uimarishaji wa kundi hilo huku likijipanga kufanya mashambulizi kuelekea Israel.

Mashambulio  ya jana ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi kuripotiwa mashariki mwa Lebanon katika wiki za hivi karibuni na yanahatarisha makubaliano dhaifu ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi hilo la Hezbollah yaliosimamiwa na Marekani, ambayo tayari yanakabiliwa na utata kutokana na tuhuma za mara kwa mara za ukiukaji.