Israel yachochea Moto unaowaka-Reccep Erdogan | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Mgogoro wa Mashariki ya kati

Israel yachochea Moto unaowaka-Reccep Erdogan

Rais wa Uturuki asema Israel inatumia fursa ya tangazo la Trump la kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel kuendeleza matumizi ya mabavu na uonevu dhidi ya wapalestina

Marais wa Uturuki na Urusi wametoa msimamo wao unaofanana juu ya suala la Marekani kuutambua Jetrsalem kama mji mkuu wa Israel. Erdogan na Putin wamesema wanaipinga hatua hiyo iliyochukuliwa na Donald Trump. Kadhalika hatua ya Trump inapingwa pia na Umoja wa Ulaya.

Rais Vladmir Putin wa Urusi na mwenzake Recep Tayyip Erdogan wamefanyaka mkutano wa pamoja na waandishi habari na kuzungumzia kuhusu msimamo wa nchi hizo mbili dhidi ya hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na rais wa Marekani Donald Trump ya kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel. Ergodan na Putin wakizungumza mjini Ankara wameonesha mtazamo wa pamoja kwamba  uamuzi wa Trump utavuruga hali ya utulivu katika Mashariki ya kati na kukwamisha juhudi za amani kati ya Israel na Palestina. Kadhalika Erdogan amesema Uturuki haitofautiani kimtazamo na Urusi  akisema kwamba wanaamini Israel inaitumia Marekani kuendelea kuchochea moto unaowaka.

Erdogan alitoa kauli nzito dhidi ya Trump

"Kimsingi Israel inaendelea kuchochea moto. Israel inayaona matukio ya hivi karibuni kama fursa ya kuongeza shinikizo  na matumizi ya nguvu dhidi ya wapalestina.Kwa mtu yoyote mwenye akili zake,maadili na busara  sio rahisi kuwapuuza wauaji hawa. Kama mnavyofahamu kama rais wa awamu wa jumuiya ya OIC tumewaalika viongozi wa nchi za kiislamu katika mkutano wa kilele na tutakutana Istanbul kwa siku mbili.Nataraji kwamba tutao ujumbe mzito. Bwana Putin na mimi tumeona kwamba tunamtazamo unaofanana kuhusu suala la Jerusalem.''

Lakini hata kabla ya Putin kuwasili Uturuki jana jioni,tayari mwenyeji wake Erdogan alitoa kauli nzito dhidi ya Trump kupitia hotuba yake aliyoitowa mjini Ankara akisema kwamba Marekani ni mshirika wa kumwaga damu. Kwa upande mwingine rais huyo wa Uturuki baadae jioni akiwa na mwenzake wa Urusi alisema wazi wazi kwamba Israel inatumia msimamo wa serikali ya Trump kama sababu ya kuonegeza shinikizo na matumizi ya nguvu dhidi ya wapalestina.

Viongozi hao wamebaini kwamba uhusiano kati ya nchi zao ni muhimu na wenye maana kwa ajili ya uthabiti wa kanda hiyo. Kiongozi wa Uturuki akasisitiza kwamba wanashirikiano na Urusi kutafuta suluhisho la kudumu la kisiasa katika mgogoro unaoendelea nchini Syria. Juu ya hilo Erdogan amefahamisha kwamba makubaliano ya serikali yake ya kununua mfumo wa ulinzi wa Makombora kutoka Urusi aina ya S 400 ambao unawatia wasiwasi washirika wa Uturuki wa NATO utakamilika wiki hii.

Maandamano yameshuhudiwa tangu Jumatatu

Putin amekwenda Ankara akitokea Cairo Misri ambapo jana pia alizungumza na rais Abdel Fatah al Sisi ambaye pia alitoa msimamo wa nchi yake kuelekea suala la Jerusalem na kusema kwamba Misri inasimama pamoja na Palestina. Hayo yamekuja katika wakati ambapo pia rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya ndani ya Wapalestina Jana hiyo hiyo alikutana na rais huyo wa Misri  kabla ya mkutano wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano ya nchi za Kiislamu utakaofanyika kesho Jumatano mjini istanbul ambako pia atashiriki.

Wakati huohuo maandamano yameshuhudiwa tangu Jumatatu katika eneo hilo la mashariki ya kati kwa siku ya tano kupinga tangazo la Trump huku ulimwengu ukiendelea vile vile kulaani msimamo huo. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini alimtakia wazi wazi waziri mkuu Netanyahu aliyekutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja huo wa Ulaya kwamba Umoja huo katu hatothubutu kuunga mkono Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Mogherini amemwambia Netanyahu ni bora akaweka matumaini yake kwa wengine na sio katika Umoja huo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba. ap,rtr

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com