1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS yadai kumchinja mwanahabari wa Marekani

20 Agosti 2014

Wapiganaji wa Jihadi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS, wametoa video inayoonyesha mwandishi wa habari wa Marekani aliyetekwa nyara nchini Syria, akichinjwa

https://p.dw.com/p/1CxPS
James Foley Journalist Reporter Libyen
Picha: dapd

Kitendo hicho kinaonekana kuwa ni hatua ya moja kwa moja ya kulipiza kisasi mashambulizi yakutokea angani yanayofanywa na Marekani nchini Iraq.

Wakati wito ukiendelea kutolewa wa Marekani kuiimarisha operesheni yake ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu – IS, kundi hilo la jihadi limetishia kumuua mwandishi mwingine wa habari wa Marekani kama mashambulizi dhidi yao hayatositishwa.

Video iliyowekwa kwenye mtandao wa Internet imemwonyesha mpiganaji aliyefunika uso wake akimchinja mwanamme anayefanana na James Foley, ambaye alitoweka baada ya kuchukuliwa mateka nchini Syria Novemba 2012.

Irak dementiert Gefahr durch Staudamm bei Mossul
Bwawa la Mosul lililokombolewa na wanajeshi wa Kikurdi kutoka mikononi mwa wanamgambo wa ISPicha: picture-alliance/dpa

Mamake Jim amesema kwenye ukurasa wake wa Facebook, kuwa walijivunia mtoto wao kwa sababu aliyatoa maisha yake wakati akijaribu kuuonyesha ulimwengu mateso wanayoyapitia wtau wa Syria. Amewaomba watekaji nyara kuwaachilia mateka wengine waliosalia mikononi mwao kwa sababu hawana hatia na hawana mamlaka yoyote kuhusiana na sera za serikali ya Marekani nchini Iraq, Syria na kwingineko Ulimwenguni.

Ikulu ya White House imesema maafisa wa uajsusi wa Marekani wanaitathmini video huyo na tayari rais Obama amejulishwa kuhusu kisa hicho baada ya kurejea mjini Washington kutoka likizoni.

Katika video hiyo ya karibu dakika tano iliyopewa kichwa “Ujumbe kwa Marekani” kundi hilo linasema Foley aliuawa kwa sababu Obama aliamuru mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya IS kaskazini mwa Iraq.

Irak Jesiden Flucht 9.8.2014
Hali ya kiutu ni mbaya kaskazini mwa Iraq, huku maelfu wakitoroka makwao kwa kuhofia kuuawaPicha: REUTERS

Alizungumza lafudhi ya Uingereza

Muuwaji huyo alisikika akizungumza kiingereza cha lafudhi ya Uingereza, na Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond amesema uchunguzi unaendelea ili kubainisha ukweli huo. "Tuna hofu kuwa muuaji huyo huenda ni raia wa Uingereza na tunalichunguza sana suala hilo. Mashirika yote yananafanya juu chini kuithibitisha video hiyo ili kuhakikisha kuwa ni ya kweli, na inahuzunisha kuwa ni ya kweli, na kisha tuone kama tunawezua kumtambua muuwaji huyo".

Baada ya kumuua mwandishi huyo, mpiganaji huyo kisha anatishia kumuua mwanamme mwingine anayeonyeshwa kwenye video hiyo akidaiwa kuwa ni Steven Sotloff, ambaye kutekwa nyara kwake mnamo Agosti 2013 hakujaripotiwa sana.

Habari za kuuliwa mwandishi huyo wa habari zimekuja wakati mashambulizi ya kutokea angani ya Marekani yalionekana kufua dafu, baada ya kuyasaidia majeshi ya Kikurdi na ya serikali ya Iraq kuwarudisha nyuma wapiganaji wa IS kutoka katika maeneo yaliyokombolewa kaskazini mwa Iraq, ikiwa ni pamoja na bwawa muhimu la Mosul.

Obama anasisitiza kuwa kiwango cha mashambulizi hayo kitasalia kuwa kidogo lakini maafisa wa Iraq na waangalizi wanahoji kuwa ni uingiliaji wa jeshi la kigeni pekee ambao unaweza kusaidia kuwaangamiza wapiganaji hao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu