Iran yakiri watu ′walidangaywa′ taarifa za ajali ya ndege | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IRAN

Iran yakiri watu 'walidangaywa' taarifa za ajali ya ndege

Iran imekiri kwamba watu walidangaywa juu ya kudunguliwa kimakosa kwa ndege ya Ukraine kulikowauwa watu wote 176 waliokuwemo, huku rais wa nchi hiyo akilitaka jeshi kuomba radhi na kufafanuwa kilichotokea.

Kauli hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, akiwa mjini New Delhi ni ya kwanza kutolewa na afisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo kusema kuwa taarifa za awali zilizodai makosa ya kiufundi ndiyo yaliyoiangusha ndege hiyo inayomilikiwa na Shirika la Ndege la Kimataifa la Ukraine zilikuwa ni uongo.

Tangu serikali ya Iran kukiri kuiangusha ndege hiyo kimakosa, kumekuwa na maandamano makubwa ya watu wenye hasira nchini humo. 

"Siku za hivi karibuni, watu wamekuwa wakiingia mitaani mjini Tehran kuandamana kutokana na ukweli kwamba walidanganywa kwa siku kadhaa," alisema Zarif.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni alilipongeza jeshi la nchi yake kwa kuwa na ujasiri wa kukiri na kuomba radhi mapema, baada ya uchunguzi kuthibitisha ukweli. 

Hata serikali ilifichwa ukweli?

Teheran Hassan Ruhani Präsident Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anataka waliohusika na ajali ya ndege wawajibishwe mara moja.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Zarif, Rais Hassan Rouhani alikuja kufahamu kuhusu kile hasa kilichotokezea siku ya Ijumaa, jambo linalozusha maswali juu ya kiasi gani serikali ya kiraia ya Iran ina nguvu mbele ya mfumo wa kitawala ambapo tabaka la viongozi wa juu wa Kishia ndilo lenye sauti ya mwisho. 

Kikosi maalum cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, ambacho ndicho kilichoiangusha ndege hiyo, kilijuwa muda huo huo kwamba kimefanya kosa, kwa mujibu wa taarifa za ndani.

Lakini kikosi hicho kinawajibika moja kwa moja kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, na sio kwa Rais Rouhani.

Ijumaa ya wiki hii, Ayatullah Khamenei ataongoza swala ya Ijumaa ya kwanza tangu hasira za umma zipande dhidi yake tangu kuangushwa kwa ndege hiyo.

Kwa miaka mingi, Wairani hawakuwahi kuhoji waziwazi mamlaka ya uongozi wa juu wa Kishia, lakini msiba mkubwa uliotokana na ndege hiyo kuangushwa umebadilisha hali ya mambo, wanasema wachambuzi.

Rouhani ataka uwajibikaji zaidi

Iran Ukraine Airlines-Absturz | Gedenken in Teheran

Mishumaa ikiwashwa kuomboleza wahanga wa ajali ya ndege ya Ukraine iliyotunguliwa kimakosa nchini Iran.

Hayo yakijiri, Rais Rouhani alilitutubia baraza lake la mawaziri siku ya Jumatano (15 Januari), ambapo alitoa wito wa umoja wa kitaifa baada ya ajali hiyo ya ndege, akisema kwamba mamlaka zinapaswa kuhakikisha kwamba zinawatendea wananchi haki.

"Watu wanataka kuona kwamba serikali inakaa nao kwa uaminifu, heshima na uadilifu," alisema Rouhani kwenye hotuba hiyo iliyotangazwa moja kwa moja na televisheni ya taifa, ambapo pia alilitolea wito jeshi kuomba radhi na kuelezea kwa undani kile hasa kilichotokezea kwenye ajali hiyo.

Tayari mamlaka nchini Iran zimeshawakamata watu kadhaa wanaohusika na ajali hiyo, lakini pia imewatia nguvuni watu wengine 30 waliokuwa kwenye maandamano ya kulaani utunguliwaji wa ndege hiyo.