Imam Mali aunga mkono rais wa kiraia wa mpito | Matukio ya Afrika | DW | 10.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Imam Mali aunga mkono rais wa kiraia wa mpito

Imamu mwenye ushawishi mkubwa nchini Mali, Mahmoud Dicko amelitolea mwito jeshi la uasi kuheshimu matakwa ya viongozi wa Afrika Magharibi ya kumteua rais wa kiraia na waziri wake mkuu ifikapo Septemba 15

Siku ya Jumamosi viongozi wa kijeshi walianza mazungumzo na vyama vya siasa vya Mali pamoja na makundi ya asasi za kiraia kwa ajili ya kipindi cha mpito cha utawala wa kiraia. Hatua hiyo ilipongezwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, ingawa vikwazo vilibaki palepale.

Dicko ambaye ni mhubiri wa Kiislamu wa madhehebu ya Salafi na ambaye mapema mwaka huu aliungana na waandamanaji wakati wa maandamano ya kuipinga serikali, aliieleza televisheni ya taifa Jumatano jioni kuwa Mali inahitaji usaidizi na kwamba haitoambulia chochote endapo itakwenda kinyume na jumuiya ya kimataifa. Soma zaidi: Hatua ya Jumuiya ya ECOWAS yakosolewa nchini Mali

"Kama jumuiya ya kimataifa, ikiwemo ECOWAS inafikiri kwamba rais wa kipindi cha mpito anapaswa kupewa raia, basi tuwape raia," alisema Imam huyo huku akijiengua katika uwezekano wa kuchukua nafasi hiyo. "Mali imejaa wakurugenzi, watu walio na uadilifu, tumtafute mtu anayefaa" alimalizia mhibiri huyo.

Rais Ibrahim Boubakar Keita alijiuzulu na kulivunja bunge mwezi uliopita baada ya kukamatwa na wanajeshi. Hatua ya wanajeshi kuchukua mamlaka ilipokelewa kwa shangwe kubwa na raia wa Mali ambao wamechoshwa na ghasia za wanamgambo wa Kiislamu na wale wa kikabila bila kusahahu kiwango kikubwa cha ufisadi.

Mali politische Krise | Vermittler Goodluck Jonathan aus Nigeria

ECOWAS wanataka serikali ya kiraia kuongoza kipindi cha mpito Mali

Makundi ya upinzani pia yalipaza sauti ya kuunga mkono mapinduzi, lakini shauku yao ilionekana kufifia wiki chache zilizopita wakati muungano wa upinzani ambao Dicko ndio kiongozi mwandamizi, kulipolikosoa vikali jeshi la uasi kwa kutowaalika katika mazungumzo ya awali juu ya kipindi cha mpito. Soma zaidi:  ECOWAS yataka utawala wa kiraia kurejeshwa Mali

Mataifa yaliyo na nguvu yanahofia kwamba kukosekana kwa utulivu wa kisiasa nchini Mali kunaweza kudhoofisha mapambano katika kanda ya Sahel dhidi za wanamgambo wa Kiislamu walio na mafungamano na makundi ya Al Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu IS, kama ilivyokuwa kwa mapinduzi ya mwaka 2012.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, Dirran Kone siku ya Jumatano wapiganaji wa jihadi waliwaua askari wanne wa Mali na kuharibu magari mawili katika shambulizi lililofanyika karibu na eneo la Alatona kwenye mkoa wa Segou katikakati mwa Mali. Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo. Eneo la Mali ya kati limekuwa kitovu cha mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi pamoja na ghasia za kikabila.

Hili ni shambulizi la nne dhidi ya vikosi vya usalama vya Mali tangu jeshi lilipomuondoa madarakani Rais Keita Agosti 18. Jumla ya askari 22 wameuwa. Hao ni sehemu tu ya mamia ya askari ambao wamepoteza maisha tangu ghasia za kisiasa na wanamgambo kuibuka katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo tangu mwaka 2012. Ghasia hizo zimeenea pia katika nchi jirani za Niger na Burkina Faso licha ya Ufaransa kupeleka wanajeshi wake.

reuters