Hatua ya Jumuiya ya ECOWAS yakosolewa nchini Mali | Matukio ya Afrika | DW | 08.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hatua ya Jumuiya ya ECOWAS yakosolewa nchini Mali

Jumuiya ya ECOWAS imetowa mwito wa kuitaka Mali kuchukua hatua ya kuyakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia ifikapo septemba 15.Hatua ya ECOWAS imepokelewa kwa shingo upande na raia wa Mali.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za ukanda wa Afrika Magharibi ECOWAS imetowa tamko la mwito wa kuitaka Mali kuchukua hatua ya kuyakabidhi kwa amani madaraka kwa utawala wa kiraia ifikapo septemba 15. Jumuiya hiyo iliiwekea vikwazo Mali baada ya mapinduzi ya Agosti 18 ikiwa ni pamoja na kufunga mipaka yake.Nchini Mali,hatua ya jumuiya ya ECOWAS imepokelewa kwa shingo upande na mashirika ya kiraia.

Kipindi cha mptito cha miezi 12

 Katika mkutano maalum wa kilele wa marais uliofanyika Jumatatu mjini Niamey, jumuiya hiyo ya Ecowas imetoa ilani ya wiki moja kwa viongozi wa kijeshi kukabidhi madaraka kwa kiongozi mpya wa kiraia.Jean-Claude Kassi Brou  Mkuu wa kamisheni ya jumuiya ya ECOWAS amesema wamesubiri utawala wa kidemokrasia nchini Mali.

''Mkutano wa marais umehakikisha tena nia yake kurejea haraka kwa utawala wa kikatiba na wa kiraia, na vile vile uteuzi wa rais na waziri mkuu wa kiraia watakaongoza kipindi cha mpito kisichozidi miezi 12''.

Hatua hiyo ya marais wa Jumuiya ya ECOWAS imekuja siku tatu kabla ya kuitishwa mazungumzo ya kitaifa, yanayoandaliwa na viongozi wa kijeshi. Mazungumzo hayo yanalenga kuweko na kipindi cha mpito kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi.

Katika juhudi za kutaka ungwaji mkono wa jumuiya ya ECOWAS, viongozi wa kijeshi walichukuwa hatua kadhaa ikiwemo kumuachilia huru Rais Ibrahim Boubacar Keita na kumruhusu asafiri kwa ajili ya matibabu kwenye Nchi za Falme za Kiarabu. Msimamo huo mkali wa jumuiya ya Ecowas dhidi ya viongozi wa kijeshi, umekosolewa nchini Mali.

''Msimamo huo ni kutaka kuturejesha nyuma''

Vuguvugu la vyama vilivyokuwa vikimpinga rais Ibrahim Keita,linafahamisha kwamba hatua ya Ecowas,inatishia usalama wa Mali. Aboubacar Sidiki Fomba, mwenyekiti wa chama cha Muungano wa watu wa Mali amesema kwamba jumuiya ya Ecowas,inashindwa kusoma nyakati.

''Jumuiya ya ECOWAS imeshindwa na vita dhidi ya ugaidi nchini Mali, inafikiria kulazimisha kuweko na utawala wa kiraia ili kujijengea sifa nzuri. Siyo chaguo la jumuiya ya ECOWAS litakaloongoza nchi ya Mali. Msimamo huo ni kutaka kuturejesha nyuma, na hilo wamedanganyika'' alisema Fomba.

Mwenyekiti wa jumuiya ya ECOWAS, rais wa Niger, Mahamadou Issoufou

Mwenyekiti wa jumuiya ya ECOWAS, rais wa Niger, Mahamadou Issoufou

Mwenyekiti wa ECOWAS, rais wa Niger,Mahamadou Issouffou, aliashiria kwamba vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Mali,vitaondolewa hatua kwa hatua. Issoufu mwanzoni amesema ni jukumu la jumuiya hiyo kuwasaidia watu wa Mali kuelekea hatua ya kurudishwa taasisi zote za kidemokrasia kwa njia ya amani.

Jumuiya ya ECOWAS iliiwekea vikwazo Mali baada ya mapinduzi ya Agosti 18 ikiwa ni pamoja na kufunga mipaka yake, na kuzuia biashara na shughuli za kifedha kutoka na kuingia nchini humo.