Wanajeshi walioasi Mali wamuachia huru Boubakar Keita | NRS-Import | DW | 28.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Wanajeshi walioasi Mali wamuachia huru Boubakar Keita

Rais wa zamani wa Mali Ibrahim Boubacar Keita amerejea nyumbani chini ya ulinzi mkali, kufuatia shinikizo kutoka kwa mataifa 15 wanachama wa ECOWAS, kutaka Keita kuachiwa huru na kurejea nyumbani.

Kulingana na familia ya rais huyo wa zamani, Ibirahim Boubacar Keita alirejea nyumbani jana jioni, baada ya kushikiliwa kwa siku 10 na wanajeshi walioasi walioipundua serikali wiki iliyopita. Keita aliye na miaka 75 alijiuzulu muda mfupi baada ya kuondolewa madarakani. 

Aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, anayehusika katika mazungumzo na wanajeshi walioasi, amesema kuachiwa kwa Keita kunaonesha wanajeshi hao wanajaribu kutekeleza matakwa ya Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, ili kuepuka vikwazo.

Jumuiya hiyo ya ECOWAS inatarajiwa kukutana hii leo kujadili mikakati mipya ya kuchukua katika mgogoro huu wa Mali. Matakwa muhimu hapa ni kwamba wanajeshi wanaoiongoza Mali waweke mara moja serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi baada ya angalau mwaka mmoja ili kurejesha utawala wa kiraia.

Lakini wanajeshi hao wanaojiita "Kamati ya kitaifa ya ukombozi wa watu wake" imependekeza kukaa madarakani kwa muda wa miaka mitatu na kusema inafanya hivyo kutokana na masuala ya usalama kufuatia mashambulizi ya makundi ya wanamgambo katika upande wa Mali ya kati na upande wa Kaskazini.

Wanajeshi wanne wauwawa kufuatia shambulio la wapiganaji wa jihadi

Hapo jana Alhamisi wanajeshi hao walitoa taarifa iliyotiwa saini na kiongozi wao Assimi Goita, inayoweka tawala za mikoa zitakazosimamia misingi ya sheria. Taarifa hiyo inaendelea kusema kuwa sheria inahitajika hasa baada ya kuvunjwa kwa bunge pamoja na serikali.

Katika tukio jengine hapo jana, jeshi la Mali lilitangaza kuuwawa kwa wanajeshi wake wanne na wengine 12 kujeruhiwa karibu na eneo la Konna Kaskazini Mashariki mwa mji wa Bamako baada ya mashambulizi makali na makundi ya jihadi.

Kikosi cha wanajeshi 13,000 cha Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika nchi jirani ya Mali kinachojumuisha wanajeshi wa Ujerumani MINUSMA, kimesema viongozi wake wamemtembelea rais wa zamani Boubakar Keita nyumbani kwake hapo jana.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian ameiambia radio ya RTL kwamba mapinduzi ya Mali hayotosimamisha operesheni za kijeshi zilizoanza mwaka 2012 zinazoongozwa na Ufaransa dhidi ya washirika wa kundi la kigaidi la al Qaeda na wanamgambo wa dola la kiislamu IS.

Siku ya Jumatano shirika la kimataifa la mataifa yanayozungmza kifaransa iliisimamisha Mali kwa muda kuwa mwanachama wake huku ikisubiri mjumbe wa shirika hilo kulitembelea taifa hilo hivi karibuni.

Chanzo: DW Page