IEBC yaukatia rufaa uamuzi wa mahakama kuzuwia uchapishaji kura | Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2017 | DW | 11.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

KENYA YAAMUA

IEBC yaukatia rufaa uamuzi wa mahakama kuzuwia uchapishaji kura

Siku 28 kabla ya uchaguzi mkuu, Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi nchini Kenya (IEBC) imekata rufaa juu ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kusitisha mchakato wa kuchapisha karatasi za kupigia kura ya rais.

Katika taarifa iliyosambazwa kwa waandishi wa habari siku ya Jumanne (11 Julai), mkurugenzi wa mawasiliano wa IEBC aliweka bayana kuwa wanaukata rufaa uamuzi huo, baada ya hapo Ijumaa Mahakama Kuu kuamua kusitishwa kwa shughuli za kuchapisha karatasi za kupigia kura ya rais.

Sababu ya hatua hiyo imetokana na umma kutoshirikishwa katika mjadala kuhusu kampuni ipi ilipaswa kupewa zabuni ya kuchapisha karatasi hizo kama yalivyo matakwa ya sheria za nchi.

Kimsingi shughuli za kuchapisha karatasi za kura kwa uchaguzi wa nyadhifa nyengine kama za wawakilishi wa wanawake, wabunge, wawakilishi wa wadi, seneta na magavana, zinaendelea.

Iwapo IEBC itasaka mzabuni mpya kuchapisha karatasi za kupigia kura ya rais, masuala mapya yatajitokeza, mojawapo likiwa la muda, kwani shughuli hiyo inahitaji muda wa siku 45 na zimesalia 28 pekee kabla uchaguzi mkuu kufanyika mwezi ujao.

Kwa mujibu wa ratiba ya IEBC, karatasi za kupigia kura ya rais zinapaswa kuanza kuchapishwa kabla mwanzo wa Agosti hii.

Kwa upande mwengine, ingawa maandalizi ya uchaguzi hayajasitishwa, wasiwasi mpya umejitokeza kuhusu idadi ya vituo vya kupigia kura na jinsi vilivyoteuliwa.

Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya vituo vya kupigia kura ni 40,000 ingawa wengine wanatilia shaka uwezo wake wa kuwahudumia wapigakura takribani milioni 20 hapo Agosti 8.

IEBC inajiandaa hapo kesho kuyajadili maoni ya umma juu ya zabuni ya kuchapisha karatasi za kupigia kura kwa wadhifa wa rais, ingawa ilishaonya kuwa haitasitisha mchakato wa uchapishaji wake.

Hapo jana, tume hiyo ilikutana na wagombea 6 wa urais na wawakilishi wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA, Raila Odinga, lakini hakuna chochote kilichotajwa kuwa suluhisho la mzozo wa kura za rais.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef
 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com