1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

ICC kutoa uamuzi rufaa ya mbabe wa kivita wa kundi la LRA

15 Desemba 2022

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, inatarajiwa kutoa uamuzi juu ya rufaa iliyokatwa na mbabe wa zamani wa kivita wa kundi la waasi la Lord Resistance Army, LRA, Dominic Ongwen.

https://p.dw.com/p/4Kxpm
Niederlande | Prozess Dominic Ongwen | Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag
Mbabe wa kivita wa kundi la LRA la nchini Uganda, Dominic OngwenPicha: ICC-CPI/REUTERS

Uamuzi wa rufaa ya Ongwen utatolewa mchana huu kwenye makao makuu ya Mahakama ya ICC mjini The Hague nchini Uholanzi.

Duru kutoka eneo yalipo majengo ya mahakama hiyo zinasema ulinzi umeimarishwa kuelekea uamuzi huo ambao yumkini utasomwa kwa muda saa kadhaa.

Dominic Ongwen alikuwa mbabe wa kivita aliyeingizwa kwenye kundi la waasi wa LRA wa nchini Uganda akiwa mtoto na kisha alipanda ngazi na kufikia wadhifa wa kamanda mwenye usemi kwenye kundi hilo.

Baada ya kesi iliyoendeshwa kwa miezi kadhaa tangu kukamatwa kwake, mwezi Februari mwaka jana majaji wa mhakama ya ICC walimkuta na hatia ya mashtaka 61 ikiwemo mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watu katika hali ya utumwa. 

Alihukumiwa kwenda jela miaka 25 mnamo mwezi Mei mwaka 2021.

Upande wa utetezi wasema Ongwen alikuwa mhanga wa vita

Den Haag | ICC verurteilt Warlord Dominic Ongwen aus Uganda
Jopo la majaji wa ICCPicha: ICC/AA/picture alliance

Kwenye uamuzi wa wakati huo, majaji walisema Ongwen binafsi alitoa amri kwa wapiganaji wake kuwauwa watu wapatao 130 katika kambi za wakimbizi kati ya mwaka 2002 na 2005.

Mkuu wa jopo la majaji waliosikiliza kesi hiyo Bertram Schmitt alikiri wakati huo kwamba walikabiliana na hali isiyo ya kawaida, kwa sababu mbabe huyo wa kivita, alikuwa ni mhanga na mhalifu kwa wakati mmoja.

Hoja hiyo ya kwamba Ongwen alikuwa mhanga imetumiwa kwa kiasi kikubwa na mawakili wake kuwarai majaji wanaosikiliza rufaa yake kubadili uamuzi wa mwaka jana uliomhukumu kifungo cha miaka 25 gerezani.

Wanasema ukweli kwamba Ongwen alikamatwa kwa mabavu akiwa mwanafunzi na kulazimishwa kujiunga na kundi la LRA ni kovu linalotosha kumwondolea hatia ya makosa aliyoyatenda.

"Dominic Ongwen alikuwa na bado hadi sasa ni mtoto” alikaririwa wakili wake Krispus Ayena Odongo akiiambia mahakama mwezi Februari mwaka huu.

Waendesha mashtaka wanasema Ongwen anabeba dhima kwa aliyoyatenda

Hata hivyo hoja hizo hazikubaliki na upande wa waendesha mashtaka wa kesi hiyo. 

Wao wanasema Ongwen anabeba dhima kamili ya makosa yote aliyoyatenda akiwa kamanda wa kundi la LRA linaloongozwa na Jospeh Kony.

Wamejenga hoja kuwa mbabe huyo wa kivita aliyefahamiwa pia na wengi kama "Siafu Mweupe” aliamuru mauaji ya raia wasio na hatia kwenye kambi za wakimbizi za Lukodi, Pajule, Odek na Abok mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Lord Resistance Army in Uganda
Wapiganaji wa kundi la LRAPicha: AP Photo/picture alliance

Lakini upande wa utetezi unasisitiza aliyafanya hayo chini ya shinikizo na aliyefaa kuwa kizimbani ni Joseph Kony, kiongozi wa kundi la LRA ambalo wataalamu masuala ya vita wanalitaja kuwa moja ya makundi katili kabisa ya waasi barani Afrika.

Kundi hilo lilianzishwa kiasi miongo mitatu iliyopita na Joseph Kony kupambana na utawala wa rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Lengo lake la kutaka kuanzisha taifa jipya chini ya misingi ya dini ya Kikristo, lilishuhudia wapiganaji wake wakiwaua mamia kwa maelfu ya watu, kuwalazimishia maelfu wengi kuyahama makaazi yao na kuwateka nyara  zaidi ya watoto 60,000 nchini Uganda kwenyewe, Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo, Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati.