Hofu ya kuzuka ghasia Kenya yaibuka | Matukio ya Afrika | DW | 17.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hofu ya kuzuka ghasia Kenya yaibuka

Kalenda ya maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini Kenya inakaribia kuanza, na tume ya uchaguzi nchini humo inaelezea hofu ya kuzuka kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2022.

Taifa hilo linashuhudia joto la kisiasa hasa kutokana na mgawanyiko mkubwa katika chama tawala, unaowaweka wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Rais Wiliam Ruto kwenye njia panda. 

Kati ya maswala yanayoangaziwa kwenye ratiba ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 ni mikakati ya kukabiliana na ghasia za baada ya uchaguzi, ikichukua mafunzo kutoka matukio na vurugu zlizoshuhudiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2017.

Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC, imeelezea hofu ya uwezekano wa wagombeaji kukataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi, ghasia kuibuka baada ya uchaguzi na mashambulizi dhidi ya wafanyikazi wa tume hiyo. 

Kwenye ratiba mpya iliyozinduliwa na IEBC, tume hiyo inahimiza mifumo thabiti ya usalama iwekwe. Kadhalika, changamoto ya kucheleweshwa kwa marekebisho ya baadhi ya sheria za uchaguzi, na kasoro kwenye mifumo ya kiteknolojia imetajwa.

Kenia Nairobi Opposition Proteste Polizeigewalt

Picha hii ilipigwa mwaka 2016 ikimuonyesha mtu aliyekuwa akikabiliana na polisi wakati kulipozuka machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Tume hiyo inahofia kujirudia kwa hali ya mkwamo wa kifedha iliyoshuhudiwa mwaka 2017 iliyosababisha kuchelewa kwa huduma muhimu kama vile ununuzi wa karatasi za upigaji kura za rais. Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema "Kama tume tumekuwa tukisema tuhataji kufadhiliwa katika kipindi kizima cha miaka mitano ya uchaguzi. Sasa tuko hapa, tunatarajia uchaguzi mwaka ujao, na awamu ya kwanza ya mgao wa fedha ndio imeingia.”

Wakizungumza mjini Nakuru Baraza kuu la makanisa nchini Kenya, NCCK, limeunga mkono mapendekezo ya tume ya uchaguzi, wakihimiza changamoto zilizopo zilishughulikiwe. Mwakilishi wa NCCK, Askofu Ernest Ng'eno amesema "Kama Kanisa tunatambua kwamba karne hii tunatarajia kwamba uongozi unapaswa kuwa na kiwango fulani cha masomo ili kukidhi mahitaji ya kisasa. Kwa hivyo tunaunga mkono hitaji la kiongozi kuwa na shahada ya taaluma fulani. Ingawa kuna sehemu chache ambazo zitapata changamoto.”

Tume hiyo bado inasubiri kuteuliwa kwa makamishna wanne ili kujaza pengo lililopo, mchakato wake ukiwa umeshang'oa nanga. Awamu ya kwanza ya zoezi la uandikishaji wa wapiga kura linatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu. Wafanyikazi wote wa umma wanaoazimia kugombea viti vya kisiasa wamepewa hadi Februari mwakani kujiuzulu afisini.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.