Hatimaye wabunge wa Afrika Mashariki waapishwa | Matukio ya Afrika | DW | 18.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hatimaye wabunge wa Afrika Mashariki waapishwa

Wabunge wapya wa Bunge la nne la Afrika Mashariki wameapishwa jijini Arusha baada ya sintofahamu iliyodumu kwa muda wa miezi saba toka bunge la tatu kumaliza muda wake mwezi Mei 2017.

Sintofahamu hiyo ilichagizwa na hali ya kisiasa katika baadhi ya nchi wanachama ikiwemo Kenya ambayo ilichelewa kuwasilisha majina ya wabunge wateule na Sudan kusini ikifikishwa katika mahakama ya Afrika Mashariki kwa kukiuka taratibu za msingi katika uteuzi wa majina ya wabunge wake katika Bunge hilo.

Wabunge hao wapya walikula kiapo cha kutumikia bunge hilo kwa muda wa miaka mitano ijayo ambapo watu mashuhuri na wanasiasa kutoka katika mataifa ya jumuiya hiyo walihudhuria na kutoa maoni mbalimbali kuhusu uwezo wa bunge hilo katika kusimamia masilahi ya Jumuiya na wananchi wa Afrika Mashariki.

Mwanasiasa Kipchumba Murkomen, mjumbe wa mbunge la Senet nchini Kenya alisema bunge hilo bado halijawa na nguvu ya kusimamia masuala ya msingi ya jumuiya hiyo na hivyo kuna haja ya sheria itakayolipa bunge hilo uwezo ikatengenezwa.

Kwa upande wake gavana wa wa Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya ambaye ni miongoni mwa wanasiasa kutoka nchini humo waliosindikiza wabunge wa taifa hilo, alisema kuwa bunge hilo la Afrika Mashariki linatakiwa kuwa na nguvu zaidi ya mabunge ya nchi wanachama ili kuharakisha maendeleo katika mtengamano huo.

Nao wabunge wapya wa bunge hilo linaloonekana kuwa na sura nyingi za vijana wasomi wanasema kuwa watafanya majukumu yao kwa msukumo mpya ili kuhakikisha kuwa bunge hilo linasaidia kuwezesha wananchi kuona faida za jumuiya hiyo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na DW wameonyesha kuwa bado masuala ya jumuiya hiyo hayajaweza kugusa kwa ukamilifu changamoto wanazokabiliana nazo katika sekta ya biashara na mawasiliano na kutaka bunge hilo kushughulikia kero hizo.

Mbunge mwakilishi wa Tanzania Dr.Ngwaru Maghembe anasema kuwa atahakikisha anapigania maslahi ya nchi anayoiwakilisha na jumuiya kwa ujumla ili kuleta ustawi kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

Mwandishi: Charles Ngereza

Mhariri: Mohammed Khelef