1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Hamas: Vifo vyapindukia 5,000 Gaza

23 Oktoba 2023

Wizara ya Afya huko Gaza imeeleza hii leo kuwa idadi ya Wapalestina waliouawa katika Ukanda wa Gaza imefikia sasa watu 5,087 na kwamba wengine 15,273 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa vita Oktoba 7 mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4Xv6B
Gazastreifen, Khan Younis | Schäden nach einem Israelischen Vergeltungsluftangriff
Majengo ya ghorofa yaliyoharibiwa na mashambulizi ya Israel huko Gaza (23.10.2023)Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Idadi hiyo ya vifo na majeruhi iliyotolewa na wizara ya afya haikuweza kuthibitishwa na vyanzo vingine huru. Jeshi la Israel linadai wizara hiyo huenda imezidisha kwa makusudi idadi ya waliofariki kufuatia mripuko katika hospitali huko Gaza ikiwa ni sehemu ya harakati za upotoshaji wa Hamas.

Wizara ya afya huko Gaza inadhibitiwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas, ambalo linazingatiwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.

Soma pia: Je, uhalifu wa kivita unapimwa vipi kwenye mzozo?

Madaktari wanaowatibu watoto wanaozaliwa kabla ya wakati huko Gaza wameonya kuwa takribani watoto 130 wako katika "hatari kubwa" hasa katika vitengo sita vya watoto wachanga kutokana na ongezeko la uhaba wa mafuta uliosababishwa na mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza.

Gaza Israel Nahostkonflikt l Verletzte nach Luftangriff auf ein Krankenhaus
Wauguzi wakimpokea mtu aliyejeruhiwa na kumuwahisha katika jengo la hospitali huko Gaza (17.10.2023)Picha: Reuters TV/REUTERS

Daktari Hatem Edhair, mkuu wa kitengo cha watoto wachanga katika Hospitali ya Nasser katika kiunga cha kusini mwa Gaza cha Khan Younis amesema hospitali hiyo itaishiwa mafuta ndani ya masaa 48, na kwamba endapo hawakapata mafuta, nusu ya watoto hao wako hatarini kufariki.

Soma pia: Fahamu mizani ya kijeshi kati ya Israel na Hamas

Leo hii pia, Israel imeonesha picha za video inazodai ni za mauaji dhidi ya raia yaliyofanywa na kundi la Hamas tarehe 7 Oktoba katika eneo la mpakani karibu na Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israel limesema Hamas bado inawashikilia mateka 222 huko Gaza. Waisraeli wamekuwa wakitoa wito wa kuachiwa wapendwa wao. Maayan Zin ni mama ambaye mabinti zake wawili wamechukuliwa mateka huko Gaza:

"Nataka wasichana wangu warejeshwe. Sijali ni nini kinahitajika kulipwa au kile kinachohitajika kutolewa. Ninachotaka ni binti zangu warudi."

Waandamanaji dhidi ya Israel wakamatwa Uholanzi

Niederlande, Den Haag | Internationaler Strafgerichtshof
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, The Hague UholanziPicha: Klaus Rainer Krieger/reportandum/IMAGO

Wakati huo huo, mamlaka nchini Uholanzi iliwaweka kizuizini kwa muda mchache wanaharakati 19 ambao walikuwa wakiandamana leo hii mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC,  wakimshtumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Mawaziri wa EU wasaka masuluhisho ya migogoro ya kikanda

Wanaharakati kutoka kundi la "Extinction Rebellion" walizuia daraja mbele ya mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague majira ya saa sita mchana, wakiwa wamebeba mabango yaliyosomeka "Netanyahu ni mhalifu wa vita."  Maandamano hayo ambayo hayakuvuruga shughuli za Mahakama hiyo, yamefanyika huku Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte akiwa amewasili Mashariki ya Kati kukutana na waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas.

Norway imesema iko tayari kusaidia uwezekano wa uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kivita huko Israel na Gaza na kwamba wamejitolea kufanya hilo bila kujali ni nani aliyehusika katika uhalifu huo huku ikisisitiza kuwa uhalifu wa kivita kamwe haukubaliki.