Hamas na Fatah wafikia mwafaka wa mshikamano | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Ukurasa mpya kwa Hamas na Fatah

Hamas na Fatah wafikia mwafaka wa mshikamano

Vyama hivyo viwili vimekubaliana huko Cairo kumaliza tafauti zao na kushikamana baada ya kuwa katika uhasama kwa muongo mzima kila upande ukiwa na serikali yake

Vyama viwili vya Palestina ambavyo vimekuwa katika mvutano na uhasama kwa kipindi cha muongo mmoja sasa, hatimaye vimefikia makubaliano ya amani, kufuatia mazungumzo ya kutafuta maridhiano na mshikamano yaliyosimamiwa na Misri. Mwafaka huo uliofikiwa hii leo umetangazwa na pande zote mbili.

Kiongozi wa chama cha Hamas, Ismail Haniyeh, ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzo kutangaza juu ya mwafaka huo asubuhi ya leo  akisema hatimaye wamekubaliana pamoja na chama cha Fatah kufikia mshikamano na amani.
Akitowa taarifa kuhusiana na hilo, msaidizi wa Ismail Haniyeh, Taher al-Nouno, ameongeza kusema kwamba makubaliano hayo yamefikiwa chini ya udhamini wa Misri. Hata hivyo, hakuna maelezo mengi yaliyotolewa kuhusiana na maridhiano hayo, ingawa kuna mkutano na waandishi habari uliopangwa kufanyika mchana wa leo, amesema Azzam al-Ahmad, ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Fatah ulioko mjini Cairo.

Wajumbe wa pande zote mbili, Hamas na Fatah, wamekuwa wakifanya mashauriano mjini Cairo tangu siku ya Jumanne wiki hii kujaribu kuvileta pamoja vyama hivyo na kuliweka eneo la Ukanda wa Gaza chini ya usimamizi wa mamlaka ya serikali ya Wapalestina. 

Chama cha Hamas, kinachoangaliwa kama ni kundi la kigaidi na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, kimekuwa kikiendesha serikali yake yenyewe katika eneo hilo la Ukanda wa Gaza tangu kilipolidhibiti eneo hilo kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2007.

Abkommen zwischen Hamas und Fatah (Picture-Alliance/dpa)

Wakati huo huo, serikali ya Mamlaka ya Wapalestina, ambayo inatambuliwa kimataifa na inayoongozwa na chama cha Fatah, imekuwa ikiendesha shughuli zake katika eneo linalokaliwa na Waisrael la Ukingo wa Magharibi, mjini Ramallah.

Juhudi chungu nzima za kujaribu kuzipatanisha pande hizi mbili, Fatah na Hamas, zimekuwa zikishindwa mara zote wakati kundi hilo la Hamas likionekana kuendelea kuimarika na kuzidi kujitegemea, ambapo limewahi kuingia katika vita mara tatu na Israel katika kipindi cha miaka 10.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema mazungumzo ya mjini Cairo nchini Misri yana nafasi kubwa sana ya kuleta mafanikio kutokana na ushiriki huo wa Misri. Misri inaendelea kuwa ni mshirika mkubwa wa serikali ya Mamlaka ya Wapalestina na inaendelea kuweka vizuizi katika eneo la Ukanda wa Gaza sambamba na Israel.

Gaza Hamas Fatah Palästinenser Treffen 23.04.2014 (Reuters)

Kiongozi wa serikali ya Hamas Ismail Haniyeh na mjumbe mwandamizi wa Fatah Azzam al-Ahmed

Masuala muhimu na tete katika mazungumzo ya Cairo yalikuwa ni hatma ya wanamgambo wa kundi la Hamas mjini Gaza na ikiwa kundi hilo lina nia ya kuiachia serikali ya Mamlaka ya Wapalestina usimamizi wa masuala ya  kiusalama ya ukanda huo.

Mshauri mwandamizi wa rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas, Nabil Shaath, anasema hadi sasa suala la Hamas kuachia udhibiti wa kijeshi limekuwa suala gumu mno.

Hata hivyo, mjumbe wa Hamas anayeshiriki kikao cha Cairo ambaye hakutaka kutajwa jina amesema makubaliano yaliyofikiwa yanatoa nafasi ya wanajeshi wa Mamlaka ya Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi watasimamia mpaka wa Rafah kati ya Gaza na Misri.

Na juu ya hilo, makundi yote ya Palestina yataanza mazungumzo kamili ya kina juu ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha wiki mbili zijazo, wakati Rais Mahmoud Abbas akitarajiwa kwenda Gaza katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com