1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Hali ya kiutu kusini mwa Gaza yakaribia kuwa 'mbaya zaidi'

5 Desemba 2023

Wasiwasi wa kimataifa juu ya vifo vya raia unazidi kuongezeka. Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, imeonya juu ya mateso makali wanayopita wakazi wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4ZmXS
Gazastreifen Ausweitung der Bodenoffensive auf den Süden
Kifaru cha Jeshi la Israel kikifanya doria karibu na mpaka wa Ukanda wa Gaza: 03.12.2023Picha: Menahem Kahana/AFP/Getty Images

Hali bado ni tete katika ukanda wa Gaza ambako jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi yake. Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa DW eneo hilo, hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza inakaribia kuwa 'mbaya zaidi'.

Wakati Israel ikitanua operesheni zake eneo la kusini mwa Ukanda huo, jeshi la nchi hiyo limewaambia wakaazi, ambao wengi wao walikuwa tayari wamekimbia  ghasia kaskazini mwa Gaza , wawe wanaangalia mtandaoni ili kufahamu ni maeneo gani yatakayolengwa kila siku na mashambulizi.

Mwandishi wa DW mjini Jerusalem Rebecca Ritters ameeleza kuwa watu wa Gaza wamepewa aina fulani ya ramani ambayo imegawanywa kwa miraba. Kila eneo lina namba na wameambiwa waangalie sehemu walipo kwenye ramani hiyo kutokana na namba hizo na kila siku watapewa orodha ya maeneo ambayo yatalengwa kwa mashambulizi na hivyo watu watatakiwa kuhama.

Mwandishi huyo ameongeza kuwa tatizo ni kwamba watu wa Gaza hawana sehemu ya kwenda na wanakosa mahali pa kukimbilia na kujificha. Watu wengi pia huenda wasiweze kupata mawasiliano ya intaneti ili kupokea ujumbe huo na kufahamu ni mahala gani patakuwa salama siku hiyo.

Wito wa Shirika la Msalaba Mwekundu na taarifa za UN

ARCHIV Gazastreifen | Rot Kreuz Fahrzeug
Gari la ICRC likiwasafirisha kuelekea eneo salama, Wapalestina ambao makazi yao yamebomolewa na mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza: 13.10.2023Picha: Ashraf Amra/AA/picture alliance

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Mirjana Spoljaric, ambaye aliwasili Gaza jana Jumatatu amesema mateso ya watu wa Gaza 'hayavumiliki' huku akitoa wito wa raia kulindwa kwa mujibu wa sheria za vita na kuruhusu misaada kuingia Gaza bila vikwazo.

Wito kama huo umetolewa pia na Berlin. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani Sebastian Fischer amesema wanatarajia Israel itatoa ulinzi "halisi" kwa raia wa Gaza na kwamba sio tu kuwataka raia kuondoka kwenye eneo la hatari, lakini kuhakikisha wako katika nafasi nzuri ya kupata makazi salama mahali pengine.

Soma pia: Israel yatanua vita Gaza Kusini hofu ikitawala kuhusu vifo vya raia

Kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa umesema asilimia 80 ya wakaazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema  karibu watu milioni 1.9 ikiwa ni sawa na asilimia 80 ya wakazi wote huko Gaza wameyakimbia makazi yao tangu Oktoba 7.

Israel Gaza | Flüchtlingslager des Hilfswerks der Vereinten Nationen für Palästina-Hilfswerke (UNRWA) in Khan Yunis
Familia za Wapalestiina wakiwa kwenye mahema ya shirika la UNRWA katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Khan Younis huko GAza:01.11.2023Picha: Abed Zagout/AA/picture alliance

Vituo vya UNRWA havikuepuka mashambulizi huko Gaza. Jumla ya vituo vya kazi 30 vimelengwa moja kwa moja huku 55 vikishuhudia uharibifu. Hata hivyo shirika hilo halikueleza ni nani aliyehusika na mashambulizi katika mitambo yao. Pia, takriban wafanyakazi 111 wa UNRWA  wameuawa huko Gaza tangu vita vilipozuka kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Hamas tarehe 7 Oktoba.

Vita vikiendelea, Israel imewataka raia wake kuchukua tahadhari wanaposafiri katika mataifa 80 duniani ikiwa ni pamoja na yale ya Magharibi mwa Ulaya kama Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.

Baraza la Usalama la Taifa la nchi hiyo (NSC) limechukua uamuzi wa kuzidisha viwango vya tahadhari na limetoa rai kwa raia wake kuepuka safari zisizo za lazima katika mataifa kama Eritrea, Afrika Kusini, nchi kadhaa za kiarabu na zile za Mashariki ya Kati hasa zinazopakana na Iran, kusini mwa Urusi, na nchi kadhaa za Kiislamu barani Asia.

NSC imesema tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, kumekuwa na ongezeko katika juhudi zinazofanywa na Iran na washirika wake ili kuyalenga maslahi ya Israel na kuwadhuru Wayahudi kote duniani.

Israel na Hamas wameanza tena mapigano