Hali nchini Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali nchini Somalia

Mkutano wa suluhu umeakhirishwa na damu inazidi kumwagika

default

Mkutano wa suluhu uliokua uitishwe jumatatu ijayo umeakhirishwa kwa mwezi mmoja katika wakati ambapo damu inaendelea kumwagika na wasomali wanazidi kuuhama mji mkuu Mogadishu.

Habari za kuakhirishwa mkutano wa suluhu zimethibitishwa tangu jana na msemaji wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Cairo.Samir Hosni anaeshughulikia masuala ya Afrika ndani ya jumuia hiyo,ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba serikali ya mpito ndiyo iliyoshauri mkutano huo uliokua hapo awali ufanyike April 16 ijayo,uakhirishwe.Sababu zinazotolewa ni kuzidi ukosefu wa usalama nchini Somalia.

Mapigano yaliyoripuka tangu March 29 iliyopita mjini Mogadischu kati ya vikosi vya Somalia na Ethiopia kwa upande mmoja na na wanamgambo wa kiislam na makundi mengineyo ya koo kwa upande wa pili yameshagharimu maisha ya zaid ya watu elfu moja.

Umoja wa Ulaya na jumuia ya kimataifa unafungamanisha kuitishwa mkutano huo wa suluhu na kupatiwa misaada ziada Somalia.

Katika mkutano wao wa hivi karibuni mjini Cairo,wawakilishi wa kundi la mashauriano kuhusu mzozo wa Somalia-linalowashirikisha Umoja wa mataifa,Marekani,Umoja wa Ulaya,Umoja wa Afrika,jumuia ya nchi za kiarabu na mataifa ya Igad pamoja na Uengereza,Italy,Norway,Sweeden na Tanzania,walitoa mwito wa nasaza kwa pande zinazohusika.Msemaji wa kundi hilo,Jens Odlander wa kutoka Sweeden alisema:

“Mwito wetu ni huu:sitisheni haraka mapigano na mheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha.Wakati umewadia sasa.Na sisi katika kundi la mashauriano msimamo wetu ni mmoja:Tunataka majadiliano yaendelezwe ili kusaka utaratibu wa kutia njiani makubaliano ya kuweka chini silaha.”

Wakati huo huo damu inaziidi kumwagika nchini Somalia.Watu wasiopungua 18 wameuwawa na wengine 15 kujeruhiwa jana, kufuatia mapigano kati ya koo mbili zinazohasimiana huko Diinsor,kusini magharibi ya Somalia.

Mapigano kati ya koo zinazohasimiana yamekua yakiripuka kila kwa mara nchini Somalia-nchi iliyotumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1991.

Mji mkuu Mogadischu ndio uliozama katika bahari ya mapigano.Tangu wafuasi wa mahakama za kiislam walipotimuliwa madarakani na wanajeshi wa Ethiopia,mwishoni mwa mwaka jana mapigano yamekua yakiripotiwa kila kukicha kati ya vikosi vya serikali vikisaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia dhidi ya makundi yanayobeba silaha.

Wakaazi wa Mogadishu wanaendelea kuyapa kisogo maskani yao.Mamia wameuuhama mji huo hii leo baada ya risasi kufyetulia hapa na pale na kugharimu maisha ya watu wasiopungua wanne hapo jana.

“Mapigano yameanza upya ndio maana tunakimbia.Nilikua miongoni mwa walioamua kusalia lakini hakuna matumaini kwamba amani itapatikana haraka-kwa hivyo nimeamua kukimbia pamoja na familia yangu” amesema hayo Hussein Dagare ambae ni baba wa watoto watatu.

 • Tarehe 12.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGP
 • Tarehe 12.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGP

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com