Hali nchini Pakistan | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 15.10.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Hali nchini Pakistan

Hali nchini Pakistan inazidi kuwa tete baada ya mapigano baina ya wanamgambo wa Taliban na vikosi vya usalama yaliozuka leo asubuhi katika mji wa Lahore mashariki mwa Pakistan kusababisha vifo vya watu 25.

Kituo cha Polisi kilichoripuliwa na bomu mjini Lahore,Pakistan

Kituo cha Polisi kilichoripuliwa na bomu mjini Lahore,Pakistan

Watu zaidi ya 20 waliokuwa na silaha walivamia shirika la kuu la uchunguzi-FIA, chuo cha mafunzo ya polisi cha Bedian na shule nyingine ya mafunzo ya polisi iliyopo huko Manawan. Afisa wa usalama, Meja Jenerali Shafqaat Ahmad, amesema hali kwa sasa iko chini ya uangalizi wa polisi na hakuna watu wanaoshikiliwa mateka. Meja Jenerali Ahmad amesema magaidi watano waliuawa katika eneo la Baidan, lakini hajaeleza idadi ya waliojeruhiwa miongoni mwa askari polisi. Aidha, magaidi wengine watatu walijiripua wenyewe. Afisa huyo amesema, wameona maiti tano zikiwa chini, ambapo kati ya hizo ni zile zilizouwawa katika mshambulio na vikosi vya usalama na wale waliojiripua wenyewe. Mkuu wa kikosi cha uokoaji, Dr. Rizwan Naseer amesema idadi ya watu waliouawa katika mashambulio yote matatu ni 25, miongoni mwao 10 wakiwa ni magaidi.

Mashambulio hayo yametokea siku chache baada ya kutokea hujuma katika makao makuu ya Rawalpindi, kutoa sura halisi juu ya ukubwa wa kitisho inachokabiliana nacho Pakistan kutoka kwa wanaharakati katika jimbo la Punjab ambalo ni muhimu kwa uchumi wa taifa hilo.

Serikali inasema mashambulizi mengi huandaliwa kutoka jimbo la Waziristan na kufanywa na Wataliban, wakisaidiwa na washirika wao kutoka makundi ya wanaharakati kutoka jimbo la Punjab.

Watu waliokuwa na silaha walivishambulia vituo vitatu vya polisi mjini Lahore. Watu saba akiwemo mmoja wa waliokuwa na silaha waliuwawa katika makao makuu ya mkoa ya idara wa polisi wa upelelezi ya shirikisho. Itakumbukwa mnamo mwezi Machi mwaka jana mtu mmoja aliyejitoa mhanga kwa kujiripua alilishambulia jengo hilo hilo na kuwauwa watu 21.

Mashambulizi ya Lahore yalizusha vingora kote mjini humo kutoka magari ya Polisi na ya wagonjwa.

Muda mfupi kabla ya mashambulizi hayo mjini Lahore, mtu aliyekuwa ndani ya gari moja alijiripua nje ya kituo cha polisi mjini Kohat akiwauwa watu 10.

Serikali ya Pakistan inasema hujuma kubwa ya kijeshi dhidi ya wataliban wa msimamo mkali wapatao 10.000 katika jimbo la Waziristan kusini ni jambo linaloweza kutokea wakati wowote.

Hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hizo za leo mjini Lahore, lakini wataliban walidai kuhusika katika shambulizi kwenye makao makuu ya jeshi mjini Rawalpindi hivi karibuni na kula kiapo watafanya hujuma zaidi, kulipiza kisasi kwa kuuwawa kiongozi wao Baitullah Mehsud katika hujuma ya anga iliofanywa na ndege za Marekani mwezi Agosti.

Pakistan yenye nguvu ya nyuklia inakabiliwa na shinikizo la Marekani kuitaka ichukuwe hatua kali dhidi ya wanaharakati wa Kiislamu, wakati ambao rais wa Marekani Barack Obama akizingatia kuongeza idadi ya wanajeshi wake wanaopigana Afghanistan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com