1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia inakabiliwa na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi

Angela Mdungu
8 Septemba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametahadharisha kuwa, dunia inakabiliwa na mgogoro wa mabadiliko ya tabia nchi. Ameyasema hayo katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ASEAN

https://p.dw.com/p/4W3oB
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres Picha: Sergei Bobylev/ITAR-TASS/IMAGO

Katika mkutano huo wa Jumuiya ya Mataifa ya kusini mashariki mwa Asia unaofanyika mjini Jakarta, Guterres amewataka viongozi wa jumuiya hiyo wachukue hatua kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kuunga mkono maendeleo ya kijani. 

Guterres amesema miezi ya Juni, Julai na Agosti ilivuna rekodi kwa kuwa yenye joto kali na na kwamba hali hiyo inaonesha haja ya kuongeza nguvu ya pamoja na mshikamano katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa mgogoro mbaya zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi bado unaweza kuepukika lakini muda unayoyoma hivyo haipaswi kuendelea kuupoteza.

Soma zaidi: Guterres aitaka dunia kuifanya Afrika kuwa nguvu ya nishati jadidifu

Ametoa hotuba hiyo mbele ya viongozi wa nchi 10 zinazounda Jumuiya ya ASEAN pamoja na wawakilishi wa mataifa ya Korea Kusini, Marekani, Japan, China, Urusi, India, Australia na New Zealand.

Amependekeza kuwepo kwa kile alichokiita "Mkataba wa Pamoja wa hali ya hewa" ambapo mataifa yanayotoa kiwango kikubwa cha gesi chafu yatafanya juhudi za ziada kupunguza hewa hiyo, na kwa mataifa tajiri yatahamasisha upatikanaji wa rasilimali za kifedhana kiufundi  ili kuunga mkono nchi zenye uchumi unaoinukia.

Mwaka huu, Guterres aliwahi kuwasilisha Ajenda inayotaka nchi zinazoendelea kufikisha asilimia sifuri ya uzalishaji wa hewa chafu itakapofika mwaka 2040, na kwa upade wa mataifa yanayochipukia kiuchumi yafikishe pia kiwango hicho kufikia mwaka 2050. Alizisifu nchi zinazounda Jumuiya ya ASEAN kama vile Indonesia na Vietnam kwa kwa kuanzisha ushirikiano utakaozisaidia katika mabadiliko ya kuingia kwenye mfumo wa nishati endelevu.

Chini ya mradi huo, Marekani na washirika wake zitatoa dola bilioni 29 kuisaidia Indonesia ambayo ni mzalishaji mkubwa wa makaa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Mizozo inayoendelea duniani itatuliwe

Wakati huohuo, Rais wa Indonesia Joko Widodo amewatolea wito viongozi wa dunia kutatua mizozo inayoendelea wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN.

  Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya usalama na biashara wakati kukiwa na ushindani unaoendelea kuongezeka baina ya mataifa makubwa.

Mkutano wa Jumuiya ya ASEAN unaofanyika Jakarta, Indonesia
Mkutano wa Jumuiya ya ASEAN unaofanyika Jakarta, IndonesiaPicha: Mast Irham/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo umezungumzia pia mvutano wa muda mrefu kuhusu masuala ya biashara na teknolojia, pamoja na mzozo wa bahari ya China Kusini, hatua ya viongozi wa kijeshi wa Myanmar kukataa kushirikiana na mpango wa amani wa ASEAN pamoja na hofu kuwa Korea Kaskazini inapanga kuipa silaha Urusi.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, Waziri Mkuu wa China Li Qiang na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov wamehudhuria katika mkutano huo uliofanyika katika mjini Jakarta.

Vyanzo: DPAE/RTRE