1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Gobena Dache: Jenerali wa Menelik II wa Ethiopia

Yusra Buwayhid
22 Februari 2021

Gobena Dache alikuwa jenerali wa kijeshi aliyemsaidia Mfalme Mkuu wa Ethiopia Menelik II kukamata maeneo makubwa ya kusini na kuiunganisha nchi kuwa na umoja. Lakini uongozi wa jenerali huyo haukumfurahisha kila mtu.

https://p.dw.com/p/3phyj

Gobena Dache: Jenerali wa Menelik II wa Ethiopia

Gobena Dache alikuwa nani?

Gobena Dache alikuwa ni jenerali aliyetumikia wakati wa utawala wa Sahle Mariam, Mfalme wa Shewa baadae aliyekuja kuwa Mfalme Mkuu wa Ethiopia Menekin wa Pili. Wanahistoria wanamuelezea Gobena Dache kama msaidizi wa karibu wa Menelik na pamoja walikamata maeneo makubwa yakawa chini ya utawala wa himaya ya Ethiopia.

Gobena Dache alizaliwa na kuishi wakati gani?

Gobena Dache alizaliwa mnamo mwaka 1821 na alifariki dunia baada ya kupata baridi Julai mwaka 1889, muda mfupi kabla ya Menelik kuchukuwa kiti cha mfalme mkuu wa Ethiopia.

Gobena Dache alikuwa na tabia gani?

Hakuna mengi yanayojulikana kuhusu Gobeda Dache, lakini baadhi ya wanahistoria wanamtazama kama mwanajeshi aliyetii amri hadi mwisho wa maisha yake. Kabla ya kula kiapo cha utiifu kwa Menelik, alikuwa miongoni mwa wanajeshi waasi waliokuwa wakimpinga Mfalme Mkuu wa wakati huo Tewodoros wa Pili.

African Roots | Ras Gobena Dache
Asili ya Afrika | Ras Gobena Dache

Gobena pamoja na wengine kadhaa waliokuwa na mitazamo sawa na yake walitamani kurejesha tena kile walichokiamini kuwa ni himaya inayotawaliwa na watu wenye nasaba na watu wa kale wa Ethiopia. Kwa ufupi, Gobena alikula kiapo cha kumtumikia mfalme ambaye nasaba yake inatokana na Mfalme Daud na Suleiman wa Israel mwenye haki ya kukaa kwenye kiti cha enzi. Na kwa maana hiyo, walilazimika pia kukamata maeneo ambayo inaaminika yalikuwa sehemu ya himaya ya Ethiopia ya karne ya 15, kabla ya kugawanyika kwa sababu ya kuibuka kwa falme ndogo ndogo.

Ni nini kinachomfanya Gobena Dache mtu muhimu katika historia ya Ethiopia?

Gobena Dache alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Mfalme Mkuu Menelik wa Pili. Mwaka 1865, Menelik alikamatwa na Mfalme Mkuu Tewodoros wa Pili, aliyekuwa na

hofu kuwa anapanga kumpindua. Menelik alipokimbiana baadae, alijitangaza kama Mfalme wa Shewa, eneo ambalo limekuja kujulikana kama mji mkuu wa Addis Ababa.

Haraka Gobena Dache alijiweka karibu na Menelik, ambaye alimfanya mkuu wa kasri lake na kumoa cheo cha ‘Ras'. Cheo hicho kinampa mamlaka ya maeneo kadhaa yaliyokuwa sehemu ya Ufalme wa Shewa. Alitekeleza amri zote za Menelik. Alimsaidia kuunda ushirika, kupigana vita, na kuhakikisha kuwa viongozi wa eneo hilo wanalipa ushuru na kula kiapo cha utiifu kwa Menelik.

Kwa nini Gobena Dache ni mtu wa kutatanisha nchini Ethiopia hadi leo?

Wakati kuna baadhi wanaomzingatia Gobena Dache kama jenerali aliyesaidia kuijenga himaya ya Ethiopia na muunganishaji watu, wengine unamuangalia kama mtu katili aliyekuwa na kiu ya kuteka maeneo na kuupanua ufalme wa Menelik. Hata wanahistoria wanakubaliana kwamba ushindi wa kijeshi wa Gobena mara nyingi ulipatikana kwa njia za kikatili. Hasa kwa wale waliokuwa wagumu kusalimu amri kwake.

Ufalme wa Kaffa, uliokuwa kusini-magharibi mwa Ethiopia ya leo, ulipambana na vikosi vya Gobena Dache na Mfalme Menelik kwa miaka mingi. Kwa vile anatoka katika kabila la Oromo, Dache wakati mwingine anaangaliwa kama shujaa aliyejisalimisha kwa kabila la Amhara wakati wa ufalme wa Menelik II. Mitazamo hiyo tofauti kuhusu Dache, iliyopo hadi hii leo ni ishara ya kuwepo kwa migawanyiko kati ya makabila ya Ethiopia.

African Roots | Ras Gobena Dache
Asili ya Afrika| Ras Gobena Dache

Kilitokea nini baada ya Gobena Dache kufariki dunia?

Gobena Dache inasemekana alishangilia kifo cha Mfalme Mkuu Yohannes mnamo mwaka 1889, kilichomaanisha kuwa Menelik hatimaye angeweza kukaa kwenye kiti cha Mfalme Mkuu wa Himaya ya Ethiopia. Lakini muda mfupi baadae, Gobena alifariki akiwa nyumbani kwake Entoto – eneo liliyoko Addis Ababa ya leo.

Kulingana na mwanahistoria Profesa Shumet Sishagne wa Chuo Kikuu cha Bahir Dar, jitihada za kijeshi za Gobena Dache na Menelik zimesaidia katika kuiunganisha Ethiopia, na kuioa nguvu ya kupambana na vikosi vya Italia iliyokuwa ikitaka kuitawala.

"Huu ulikuwa ni wakati ambapo mataifa mengi ya Kiafrika yalikuwa yanakabiliwa na kitisho cha kutawaliwa na Wazungu waliokuwa wanapanua himaya zao za Ulaya,” anaeleza Sishagne. "Kumbuka, kongamano la Berlin lilifanyika mwaka 1884. Na mwaka 1884, (Gobena Dache na Menelik) walikuwa tayari wameshaweza kudhibiti maeneo makubwa ya kusini na kusini magharibi mwa Ethiopia. "

Miaka michache baadaye , Jeshi la Menelik lilivishinda vikosi vya Italia katika vita vya Adwa - na kuifanya Ethiopia kuwa nchi pekee ya Kiafrika ambayo haikuwahi kutawaliwa na wakoloni.

Gobena Dache: Mshirika wa Menelik II

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.