1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Garba na Borana: Alama ya Kenya iliyogawika

10 Desemba 2013

Huku Wakenya wakiadhimisha miaka 50 ya uhuru, mauaji ya kikabila yanaonesha namna taifa hilo linavyoendelea kukabiliwa na changamoto kubwa la kupatanisha makabila na makundi yake ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/1AW5e
Watu waliochawanywa na mapigano nchini Kenya.
Watu waliochawanywa na mapigano nchini Kenya.Picha: Anjali Nayar

Majeraha matatu makubwa yanaonekana kwenye kichwa cha Abdi Isse, mvulana wa miaka 20, ambaye ni mmoja wa waliojeruhiwa katika ghasia za kikabila kaskazini mwa Kenya.

"Walitushambulia wakati wa alfajiri, wakampiga risasi kila mtu, wanawake na watoto pia, na wengine kutukana kwa mapanga," anasema jamaa yake, Adan Hassan, huku muuguzi akiwainga nzi waliozonga vidonda vya mgonjwa wake.

Mlango wa pili, kuna wanaume wengine wawili wakiuguza majeraha ya risasi, mmoja la mguuni mwengine la begani, huku minofu ya nyama zilizofumuliwa kwa risasi ikiwa wazi kule risasi zilikotokea.

Mauaji ya kikabila miaka 50 baada ya uhuru

Hii nayo ni Kenya ya miaka 50 baada ya uhuru wake kutoka kwa Muingereza. Bado Wakenya wameendelea kupigana na kuuana kugombea ardhi na maeneo ya malisho ya wanyama wao kwa misingi ya makabila yao.

Watu waliochawanywa na mapigano nchini Kenya.
Watu waliochawanywa na mapigano nchini Kenya.Picha: dapd

Miezi kadhaa ya hali ya wasiwasi iligeuka kuwa mapigano wiki iliyopita, baada ya makundi hasimu ya jamii za Gabra na Borana wilayani Moyale, kwenye mpaka wa kaskazini na Ethiopia, walipopambana.

Watu kadhaa wameuawa kwa risasi na mapanga katika eneo hilo la kaskazini, maduka yameporwa, nyumba kuchomwa moto na maelfu ya watu kulazimishwa kuyakimbia makaazi yao.

Mchango wa wanasiasa

Watu wengi wanasema hali ya mashaka kati ya makabila imekuwa ikichochewa na wanasiasa na kwenye eneo kama hilo ambalo bunduki zimeenea kila mahala, kwa vile kupakana kwake na Somalia, mapigano ni rahisi mno kuzuka.

Bado kumbukumbu chungu zimeendelea kubakia kwa ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa.

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto, hivi sasa wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakishukiwa kupanga ghasia hizo, tuhuma wanazozikana vikali.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.Picha: John Muchucha/AFP/Getty Images

Mji wa Moyale una mbunge anayetokana na jamii ya Borana, lakini kwa ujumla wilaya hiyo imekuwa ikitawaliwa na watu wa jamii ya Gabra tangu uchaguzi wa Machi. Huku utaratibu mpya wa uendeshaji nchi ukiwa unaruhusu nguvu za ziada na bajeti kwa serikali za majimbo, ushindani wa madaraka umekuwa mbaya zaidi.

"Kumekuwa na mapigano na jamii ya Borana hapo kabla, lakini hiki ni kitu tafauti, anasema Hassan, mtu mzima wa kabila la Garba.

Kwa upande mwengine, jamii ya Borana wana mtazamo huo huo. "Hawa jamaa wamekusudia hasa, wanatushambulia kwa bunduki na mabomu," anasema Adan Mohammed ambaye ndio kwanza amehitimu masomo yako ya biashara katika Chuo Kikuu cha Nairobi, akiongeza kwamba maadui zao wanachochewa na wanasiasa ili kabila lao liwe juu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman